Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma imetoa tamko rasmi ikikanusha vikali taarifa za upotoshaji zinazosambaa kwenye mitandao zinazodai kuwepo kwa shule ya msingi iitwayo “Madaba” yenye changamoto kubwa za miundombinu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Ruvuma, Bi. Mary Makondo akizungumza na wanahabari kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Ahmed Abbas, amesema, shule hiyo haipo kwenye orodha ya shule zilizosajiliwa katika Halmashauri ya Wilaya ya Madaba, na haijawahi kuwapo katika rekodi za Serikali.
Amesisitiza kuwa taarifa hizo, zina lengo la kuchafua taswira ya Serikali, na kwamba zimesababisha taharuki kwa wananchi, hasa wazazi na wadau wa elimu.
Hata hivyo amesema upotoshaji huo si mpya kwani hata mwaka 2022 video feki hiyo iliwahi kusambazwa ikionesha wanafunzi wakisomea chini ya kibanda cha miti katika shule inayoitwa Litapatile, ambayo pia haipo katika Wilaya ya Madaba wala mkoani Ruvuma.
“Mwaka 2022 Mheshimiwa Mkuu wa Mkoa alikanusha hadharani taarifa hiyo kupitia vyombo vya habari baada ya kufanya uchunguzi wa kina. Tunaendelea kusisitiza kuwa hakuna shule yoyote yenye jina la Madaba au Litapatile katika orodha ya shule zilizosajiliwa mkoani Ruvuma,” alieleza Bi. Makondo katika taarifa hiyo kwa vyombo vya habari.
Katika kuhimiza uwajibikaji na uadilifu wa kihabari, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa imetoa wito mahsusi kwa waandishi wa habari, watumiaji wa mitandao ya kijamii na jamii kwa ujumla kuhakikisha wanafanya uhakiki wa kina kutoka pande husika kabla ya kusambaza taarifa kwa umma.
Taarifa zisizokuwa na uthibitisho zimeelezwa kuwa zinavuruga amani na juhudi za Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Aidha, Ofisi hiyo imetoa onyo kali kwa watu wote wanaojihusisha na kusambaza taarifa hizo za uongo, ikibainisha kuwa ni kosa la jinai chini ya Sheria ya Makosa ya Mtandao Na. 14 ya mwaka 2015, ambapo yeyote atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Katika siku za hivi karibuni, kumekuwa na ongezeko la matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii nchini, ambapo baadhi ya watu wasio waadilifu wamekuwa wakitengeneza na kusambaza taarifa za kughushi kwa malengo ya kisiasa, kibiashara au kuvuruga amani.