Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS) Prof. Appolinary Kamuhabwa akizungumza wakati akifunga Kongamano la 13 la Kisayansi la MUHAS lililofanyika 19 Juni, 2025 katika Ukumbi wa Kituo cha Umahiri cha Magonjwa ya Moyo na Mishipa ya Damu cha Afrika Mashariki, Kampasi ya Mloganzila, Dar es Salaam.
Na Karama Kenyunko
WATAALAM wa masuala ya afya nchini wameafikiana kuwa tafiti zinazofanywa kuhusu afya zinapaswa kuwa na matokeo chanya kwa jamii, badala ya kubaki kwenye makabrasha ya kitaaluma pekee.
Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi Shirikishi Muhimbili (MUHAS), Profesa Appolinary Kamuhabwa, amesema hayo jana, Juni 19, 2025, katika Kongamano la 13 la Sayansi lililofanyika chuoni hapo.
“Katika kongamano hili kulikuwa na mawasilisho ya tafiti mbalimbali zilizolenga masuala ya afya, ikiwemo matumizi ya dawa, magonjwa, mifumo ya afya, na matumizi ya teknolojia kama vile akili mnemba (Artificial Intelligence) katika sekta ya afya,” alisema Prof. Kamuhabwa.
Alieleza kuwa tafiti hizo hazitaishia katika makaratasi, bali zitatumika kuleta mabadiliko halisi katika jamii. “Tumeunda kamati maalumu ya kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa kwa watunga sera kwa lugha rahisi na inayoeleweka, lengo likiwa ni kusaidia kupitisha sera bora za kiafya,” alifafanua.
Kongamano hilo lilihudhuriwa na watu takribani 500 kutoka nchi 11 na jumla ya tafiti 218 ziliwasilishwa. Prof. Kamuhabwa aliongeza kuwa ushiriki wa vijana ulikuwa mkubwa, hususan kwenye tafiti zinazohusisha teknolojia, jambo linaloashiria mwamko mpya katika sayansi ya afya nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Maandalizi wa Kongamano la 13 la Sayansi MUHAS Profesa Raphael Sangeda alisisitiza umuhimu wa tafiti hizo kuwafikia wananchi. “Tafiti hizi hazipaswi kuishia kwenye makabrasha. Zinapaswa kuwasaidia wananchi kubadili mtindo wa maisha, kama vile ulaji bora na kufanya mazoezi, ili kujikinga na magonjwa yasiyoambukiza,” alisema.
Naye Bhoke Juma, Mwanafunzi wa kidato cha Pili Kada ya Afya ya Sayansi na Mazingira alisema kongamano hilo limewapa wanafunzi motisha kubwa katika kufanya tafiti zenye manufaa kwa jamii.
“Tumehamasika kuendelea kujifunza na kubuni mambo mapya. Mimi binafsi nimejifunza namna ya kutambua majanga katika mazingira na jinsi ya kuyadhibiti,” alisema








