Kamishna Mkuu wa Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Kanali Burhan Zubeir Nassor, Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yao ya migombani kuhusu watuhumiwa wa madawa ya kulevya
PICHA NA FATMA KHATOR MAELEZO
NA IBRAHIM DUNIA MAELEZO TAREHE
Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar imetaifisha nyumba ya mtuhumiwa Said Seif Salum, maarufu kwa jina la Said Obama, yenye thamani ya shilingi milioni 966,000,000.00, iliyopo katika eneo la Mtendeni, Wilaya ya Mjini, kuwa mali ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar.
Akizungumza na waandishi wa habari katika ofisi yao ya migombani, Kamishna Mkuu wa Mamlaka hiyo, Kanali Burhan Zubeir Nassor, amesema kuwa hatua hiyo imechukuliwa kwa mujibu wa mamlaka aliyopewa chini ya Kifungu cha 73(1) cha Sheria ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar, Na. 8 ya mwaka 2021, baada ya kutekelezwa kwa matakwa ya Kifungu cha 71 cha sheria hiyo.
Kamishna Burhan ameeleza kuwa Mtuhumiwa huyo anatajwa kuwa miongoni mwa vinara wa mtandao wa kimataifa wa usafirishaji na usambazaji wa dawa za kulevya katika Ukanda wa Afrika Mashariki, ambapo inadaiwa kuwa amekuwa akihusika kuingiza dawa hizo kutoka Afghanistan na kuzisambaza katika nchi mbalimbali za ukanda huo.
Aidha, Mamlaka hiyo imewakamata watuhumiwa wawili waliotajwa kuwa sehemu ya mtandao huo, ambao ni Ali Mohamed Ali na Fahad Ali Khamis, waliokiri kupokea dawa za kulevya kutoka kwa Said Obama, ambaye anadaiwa kuwa na makazi Zanzibar, Dar es Salaam na Kenya.
Juhudi za kumsaka Said Obama bado zinaendelea, na Mamlaka imetangaza zawadi ya shilingi milioni 10 (10,000,000.00) kwa mtu yeyote atakayetoa taarifa zitakazosaidia kukamatwa kwake pamoja na kubainika kwa mali alizoficha ndani na nje ya Zanzibar.
Kamishna amesema kuwa operesheni ya kupambana na mitandao ya biashara haramu ya dawa za kulevya inaendelea kwa ushirikiano wa karibu na vyombo vya ulinzi na usalama, ikijumuisha hatua za kuwakamata wahusika, kuwafikisha mahakamani na kutaifisha mali zilizopatikana kupitia shughuli za kihalifu.
Katika hatua nyingine, Mamlaka imetangaza nafasi kumi (10) kwa vijana wa kujitolea, wenye umri wa miaka 18 hadi 35, waliopo tayari kuacha matumizi ya dawa za kulevya kwa hiari yao. Vijana hao watapatiwa matibabu bure pamoja na mafunzo ya stadi za maisha katika kituo cha tiba na marekebisho ya tabia kilichopo Kidimni Zanzibar.
Kamishna pia ametoa wito kwa viongozi wa dini, taasisi za kiraia, wanasiasa, wabunge na wawakilishi kushiriki kikamilifu katika mapambano haya kwa kutoa hamasa na kusaidia gharama za matibabu kwa waathirika waliopo katika maeneo yao.
Aidha, amebainisha kuwa Mamlaka iko katika wiki ya maadhimisho ya kupinga biashara na matumizi ya dawa za kulevya, kuelekea Siku ya Kimataifa ya Kupiga Vita Dawa za Kulevya, inayoadhimishwa kila mwaka tarehe 26 Juni.