Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete akizungumza wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Sheria lililofanyika leo Juni 21, 2025 katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Hamza S. Johari akizungumza wakati ufunguzi wa Kongamano la Kitaifa la Sheria lililofanyika leo Juni 21, 2025 katika Kituo cha Mikutano ya Kimataifa Julius Nyerere (JNICC), Dar es Salaam.
Baadhi ya picha za matukio mbalimbali katika Kongamano la Kitaifa la Sheria
…………..
NA NOEL RUKANUGA, DAR ES SALAAM
Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Mheshimiwa Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, amewataka viongozi, Tume ya Uchaguzi na wananchi kwa ujumla kutimiza wajibu wao ipasavyo ili kuhakikisha uchaguzi mkuu wa mwaka 2025 unakuwa huru, haki na wa kidemokrasia.
Akizungumza leo Juni 21, 2025 jijini Dar es Salaam wakati akifungua Kongamano la Kitaifa la Sheria, Dkt. Kikwete amesema kuwa kongamano hilo ni jukwaa muhimu la kubadilishana mawazo na kujenga uelewa kuhusu masuala ya uchaguzi, hivyo ni vyema wadau wote kulitumia ipasavyo kuchangia hoja zenye tija kwa mustakabali wa taifa.
“Uwajibikaji ni msingi wa uongozi unaoaminika. Kila mdau wa uchaguzi – iwe ni Tume ya Uchaguzi, wapiga kura, viongozi wa kisiasa na wananchi kwa ujumla – anatakiwa kutekeleza wajibu wake kwa uaminifu ili kuhakikisha tunapata uchaguzi wa haki na wa kuaminika,” amesema Dkt. Kikwete.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa kutoa maoni kwa uhuru bila kutumia lugha au njia zisizofaa ambazo zinaweza kuathiri mshikamano wa kijamii. Huku akivitaka vyama vya siasa na wadau wengine kudumisha umoja wa kitaifa licha ya tofauti za kiitikadi na kidini.
Dkt. Kikwete pia amelitaka Jeshi la Polisi kusimamia haki za kisiasa kwa usawa na kuhakikisha amani inatawala kipindi chote cha uchaguzi pamoja na pande zote kushindana kwa hoja zinazojenga badala ya zile zinazoligawa Taifa.
Kwa upande wake, Mlezi wa Chama cha Mawakili wa Serikali na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mheshimiwa Hamza S. Johari, amesema kuwa lengo la kongamano hilo ni kukuza uelewa wa wananchi kuhusu masuala ya kisheria yanayohusu uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Mheshimiwa Johari amebainisha kuwa mwaka 2024 kulitungwa sheria mbili muhimu – Sheria ya Uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani Na. 1 ya 2024, pamoja na Sheria ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi Na. 2 ya 2024.
Ameeleza kuwa kupitia kongamano hilo, wananchi watapata fursa ya kuelewa kwa kina mabadiliko yaliyofanyika kupitia mada zitakazowasilishwa na wataalamu wa sheria na mijadala itakayofanyika.
“Watanzania watapata nafasi ya kuuliza maswali, kujadili na kuelewa mabadiliko ya mfumo wa kisheria ili waweze kushiriki kikamilifu katika uchaguzi ujao kwa maarifa na uelewa wa kutosha,” amesema Mhe. Johari.
Rais wa Chama cha Mawakili wa Serikali Tanzania ,Bavoo Junus amesema kuwa kongamano hilo limekisudia kutoa elimu kuhusu muhimu wa wananchi kujua Sheria za uchaguzi pamoja kujengewa uelewa wA Sheria mbalimbali zinazohusiana na uchaguzi katika kipindi ambacho Taifa linaelekea kwenye uchaguzi Mkuu wa 2025.
Kaulimbiu ya kongamano hilo ni: “Demokrasia kwa Vitendo: Sheria, Uwajibikaji na Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.”