Na Silivia Amandius.
Missenyi, Kagera.
Katika hatua ya kuimarisha miundombinu ya biashara na kuinua uchumi wa wananchi, leo tarehe 20 Juni 2025, limefanyika zoezi rasmi la utiaji saini mkataba wa ujenzi wa Soko la Kisasa Bunazi, lililopo katika Wilaya ya Missenyi, mkoani Kagera. Mradi huo mkubwa unatarajiwa kugharimu zaidi ya shilingi bilioni tano kwa awamu ya kwanza na utatekelezwa ndani ya kipindi cha miezi 18, kuanzia sasa hadi mwaka 2026.
Akizungumza katika hafla hiyo, Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya ya Missenyi alieleza kuwa utekelezaji wa mradi huu ni sehemu ya juhudi za serikali za kuboresha mazingira ya biashara, kuongeza mapato ya Halmashauri na kuinua uchumi wa wananchi. Alibainisha kuwa mkataba huo umezingatia viwango vya kitaalamu vya ujenzi na matarajio ya wananchi wa Missenyi yamepewa kipaumbele.
Mgeni rasmi katika tukio hilo, Mkuu wa Wilaya ya Missenyi, Mhe. Kanali Hamisi Maiga, aliwapongeza viongozi wa Halmashauri kwa kazi nzuri na kusisitiza kuwa soko hilo ni mradi wa kimkakati ambao utasaidia kuchochea maendeleo ya wananchi wa eneo hilo. Alitoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika ulinzi na ufuatiliaji wa mradi ili kuhakikisha thamani ya fedha inaonekana katika utekelezaji.
Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Missenyi, Mhe. Florent Kyombo, aliunga mkono kwa nguvu utekelezaji wa mradi huo na kusisitiza kuwa soko hilo litakuwa nyenzo muhimu ya kuinua kipato cha wananchi, kuongeza fursa za ajira na kuchochea ukuaji wa biashara ndogondogo. Aidha, alitoa wito kwa viongozi wa serikali na jamii kuhakikisha mradi huo unatekelezwa kwa wakati na kwa ubora unaotakiwa.
Naye Mhe. Paulo Mwanga, aliwataka watendaji wa serikali kuendelea kusimamia vyema miradi ya maendeleo na kuutumia mradi huu kama chachu ya kuongeza mapato ya halmashauri na ustawi wa wananchi. Alisema ni muhimu kuhakikisha kila mwananchi anaona faida ya moja kwa moja ya uwepo wa mradi huu wa soko la kisasa.
Wananchi wa Bunazi nao hawakubaki nyuma, ambapo katika maoni yao walieleza kufurahishwa na ujio wa mradi huo mkubwa. Walisema wamekuwa wakisubiri kwa hamu soko la kisasa kwa muda mrefu, na sasa wanaamini ndoto zao zinakwenda kutimia. “Tunamshukuru sana Mbunge wetu Mhe. Kyombo kwa kusimamia maendeleo ya kweli. Soko hili litatusaidia sana kama wakulima na wafanyabiashara wadogo. Hii ni neema kubwa kwetu,” alisema Bi. Editha John, mmoja wa akina mama wa soko la Bunazi.
Wengine walieleza kuwa mradi huo utaondoa adha ya kuuza bidhaa katika mazingira yasiyo rasmi na kuboresha hadhi ya eneo hilo kiuchumi. Walitoa wito kwa viongozi kuhakikisha ushirikishwaji wa wananchi unazingatiwa katika kila hatua ya utekelezaji wa mradi.