Na Karama Kenyunko Michuzi Tv

Mkutano huo mkubwa unatarajiwa kuvutia zaidi ya washiriki 500, wakiwemo 150 kutoka mataifa mbalimbali duniani na utafunguliwa rasmi na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk Samia Suluhu Hassan.
Pia Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Hussein Ali Mwinyi, anatarajiwa kuwa mgeni maalum katika hafla ya utoaji wa tuzo maalum za kuadhimisha miaka 30 ya Baraza la Habari Tanzania (MCT).
Akizungumza na vyombo vya habari leo jijini Dar es Salaam, Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA), amesema kuwa mkutano huo utaangazia masuala muhimu ya maendeleo ya sheria za habari na mawasiliano kwa ajili ya ustawi wa uandishi wa habari barani Afrika.
“Mkutano huu unaongozwa na kaulimbiu isemayo ‘Advancing Media and Communication Regulations for Journalism Excellence in Africa’ ambayo kwa Kiswahili ina maana ya ‘Uboreshaji wa Sheria za Mawasiliano kwa Ustawi wa Uandishi wa Habari Barani Afrika’,” amesema Sungura.
Ameeleza wageni mashuhuri wanaotarajiwa kuhudhuria ni pamoja na Naibu Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO anayeshughulikia Mawasiliano na Habari, Dk. Tawfik Jelassi, pamoja na mawaziri wa sekta ya habari na mawasiliano kutoka mataifa kadhaa ya Afrika.
Baadhi yao ni pamoja na William Gitau kutoka Kenya, Profesa Palamagamba Kabudi na Jerry Silaa kutoka Tanzania, Dk Chris Baryomunsi kutoka Uganda, Cornelius Mweetwa kutoka Zambia na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki, Veronica Nduva.
Kwa mujibu wa Sungura, mkutano huo utahusisha mijadala ya kitaalamu kuhusu changamoto katika sekta ya habari, maonesho ya teknolojia na mawasiliano, pamoja na uzinduzi wa maadhimisho ya miaka 30 ya MCT.
Aidha, mikutano mingine ya kimataifa itakayofanyika ni pamoja na ya Umoja wa Mabaraza ya Habari ya Afrika Mashariki (EAPC) na ile ya World Association of Press Councils (WAPC).
Mkutano huo umeandaliwa kwa ushirikiano wa Baraza la Habari Tanzania, Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA), Umoja wa Mabaraza ya Habari ya Afrika Mashariki (EAPC), na Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.
Wadhamini wa mkutano huo ni pamoja na UNESCO, Konrad-Adenauer-Stiftung (KAS), NCAA, TANAPA, PSSSF, NMB, AZAM MEDIA, TBC, Lush Garden Hotel, KILI FAIR, MST na TARURA.
Katibu Mtendaji wa Baraza la Habari Tanzania (MCT), Ernest Sungura, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Mtandao wa Mabaraza Huru ya Habari Afrika (NIMCA) akizungumza na waandishi wa habari hawapo pichani juu ya mkutano wa Kimataifa wa Mabaraza ya Habari Afrika utakaofanyika kwa siku nne kuanzia Julai 4 hadi Julai 17 2025 Jijini Arusha.