Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu Bw.Conrad Millinga, akizungumza na Waandishi wa habari katika Banda la Ofisi hiyo wakati wa Maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yaliyomalizika Leo Juni 23,2025 katika Viwanja vya Chinangali Park Jijini Dodoma.
Na Alex Sonna,Dodoma
Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu imesema imeitumia vyema Wiki ya Utumishi wa Umma ambayo ilianza Juni 16 na kuhitimishwa Juni 23, 2025 kwa kuelimisha wananchi kuhusu majukumu yake na fursa mbalimbali zinazopatikana kupitia ofisi hiyo.
Akizungumza na vyombo vya habari jijini Dodoma, Mkurugenzi wa Idara ya Uwezeshaji Kiuchumi na Maendeleo ya Sekta Binafsi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu – Sera, Bunge na Uratibu Bw.Conrad Millinga, amesema wananchi walipata nafasi ya kufahamu kwa undani shughuli mbalimbali zinazoratibiwa na ofisi hiyo, ikiwemo mifuko ya uwezeshaji kiuchumi, programu za maendeleo, na sera mbalimbali za kiuchumi zinazolenga kuimarisha maisha ya Watanzania.
“Tumetoa elimu kuhusu fursa zilizopo kupitia mifuko ya uwezeshaji kiuchumi na namna wananchi wanavyoweza kunufaika na programu mbalimbali za kitaifa,lengo ni kujenga uelewa ili kuwawezesha Watanzania kushiriki kikamilifu katika maendeleo ya taifa,” amesema Millinga.
Aidha, ameeleza kuwa ofisi hiyo imekuwa mstari wa mbele kuelimisha jamii juu ya matumizi sahihi ya alama za Taifa kama vile Bendera ya Taifa, Wimbo wa Taifa, na Ngao ya Taifa.
Amefafanua kuwa baadhi ya taasisi na watu binafsi wamekuwa wakitumia alama hizo kwa njia isiyo sahihi kinyume na taratibu zilizowekwa.
“Tumeona matumizi yasiyo sahihi ya alama hizi muhimu, kwa mfano, wimbo wa taifa hauimbwi kwa ukamilifu wake. Tunaeleza kuwa ni lazima kuimba beti zote mbili kama ilivyoainishwa,
Pia, matumizi ya rangi na michoro ya bendera au ngao lazima yaendane na muundo rasmi uliowekwa,” anasisitiza.
Katika upande mwingine, Mkurugenzi huyo amesema wananchi walipata elimu kuhusu Idara ya Menejimenti ya Maafa, ambapo walifahamishwa juu ya sera mpya ya mwaka 2025 inayotoa mwongozo wa kisekta kuhusu namna bora ya kukabiliana na maafa nchini.
Amebainisha kuwa idara hiyo ina mfumo wa kisasa wa tahadhari za mapema, unaotambua dalili za majanga kabla hayajatokea na kutoa taarifa kwa wananchi kwa wakati.
Vilevile, Millinga ameeleza kuwa wananchi walipata maelezo kuhusu Idara ya Ufuatiliaji na Tathmini, ambayo kwa sasa ina jukumu la kuhakikisha utekelezaji wa shughuli za Serikali unafuatiliwa na kutathminiwa kwa wakati, kwa lengo la kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma.
Katika hatua nyingine Millinga ametoa wito kwa wananchi kuendelea kujitokeza kupata elimu zaidi katika Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yatakayofanyika kuanzia Juni 28 hadi Julai 13, 2025 katika viwanja vya Sabasaba, Dar es Salaam.
“Tutakuwa na banda la Ofisi ya Waziri Mkuu linalojumuisha Taasisi zake zote, ikiwemo Sera, Bunge na Uratibu, Ofisi ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, ambapo tutatoa elimu kuhusu huduma zote zinazotolewa,” amesema.
Amesema wananchi watakaotembelea banda hilo watapata taarifa sahihi na fursa mbalimbali za kiuchumi na kijamii zinazotolewa na Serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu na taasisi zake na kwamba Ushiriki wao ni hatua muhimu katika kuchochea maendeleo jumuishi na yenye tija kwa Taifa.