Na Mwandishi Wetu, Iringa
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji (NIRC) imesema kuwa jitihada kubwa za Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan zimekuwa mkombozi wa wakulima na nguzo ya mapambano dhidi ya athari za mabadiliko ya tabianchi, kupitia uwekezaji mkubwa kwenye miundombinu ya umwagiliaji.
Akizungumza katika mkutano maalum ulioandaliwa na NIRC kwa kushirikisha wahariri wa vyombo vya habari nchini, Mkurugenzi Mkuu wa tume hiyo, Raymond Mndolwa alisema Serikali imetoa takriban Sh. trilioni 1.2 katika kipindi cha miaka mitatu, fedha ambazo zimewezesha utekelezaji wa miradi mipya ya umwagiliaji na kuimarisha usimamizi wa rasilimali maji kwa ajili ya kilimo.
“Tumejipanga kuhakikisha wakulima wanapata maji ya uhakika kwa kilimo, hata katika vipindi vya ukame, kwa kujenga mabwawa, kuchimba visima na kuendeleza miundombinu ya kimkakati katika mabonde 22 nchini,” alisema Mndolwa.
Alibainisha kuwa bajeti ya tume hiyo imeongezeka kwa kasi kutoka Sh. bilioni 51.49 mwaka 2021/2022 hadi Sh. bilioni 403.78 mwaka 2024/2025, sawa na ongezeko la asilimia 684.19, hatua ambayo imeiwezesha tume hiyo kuongeza eneo la kilimo cha umwagiliaji kutoka hekta 461,000 hadi hekta 983,466.06.
Kwa mujibu wa Mndolwa, lengo ni kufikia hekta milioni tano zinazomwagiliwa ifikapo mwaka 2030, huku uzalishaji wa mazao ukiongezeka na kuchangia kwa kiasi kikubwa katika pato la taifa.
“Tuna matarajio makubwa kwamba ajira zitazidi kuongezeka kupitia sekta hii, huku kipato cha mkulima mmoja mmoja kikiongezeka kwa kasi kupitia kilimo chenye tija,” aliongeza.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Nchini (TEF), Deodatus Balile aliipongeza NIRC kwa hatua kubwa iliyopiga, akisisitiza kuwa kilimo cha umwagiliaji ni silaha ya taifa katika kuhakikisha usalama wa chakula.
“Mmefanya kazi nzuri. Jitihada hizi ni kielelezo cha dhamira ya Serikali kuifanya Tanzania kuwa taifa lisilo na njaa,” alisema Balile.
Naye Mwenyekiti wa TAMWA, Joyce Shebe alisema kilimo cha umwagiliaji kimeleta mageuzi kwa wakulima wengi hasa wanawake, kwa kuwawezesha kulima katika msimu wote na kupata chakula na kipato cha uhakika.
“Ni mkombozi mkubwa kwa wakulima wetu. Kwa sasa wanaweza kulima bila kutegemea mvua za msimu,” alisema Shebe.
Kwa ujumla, maendeleo haya yanadhihirisha kwamba umwagiliaji si tu njia ya kuongeza uzalishaji, bali ni mbinu ya kimkakati ya kujenga uchumi shindani, wenye uwezo wa kukabiliana na changamoto za hali ya hewa na kupunguza umasikini vijijini.