Tunduru – Ruvuma.
Wakulima wa zao la ufuta katika Wilaya ya Tunduru wameonyesha kuridhishwa na mchakato wa mauzo kupitia mfumo wa mnada wa wazi, ambapo kilo 604,613 za ufuta, sawa na tani 604.6, zimeuzwa kwa bei ya wastani ya shilingi 2,492 kwa kilo.
Mnada huo wa nne umefanyika leo katika kata ya Nakayaya, kijiji cha Nakayaya, na kuendeshwa na Chama Kikuu cha Ushirika Tunduru Ltd (TAMCU) kwa mafanikio makubwa, Bei ya chini ilikuwa shilingi 2,440 huku bei ya juu ikiwa shilingi 2,510 na bei ya wastani shilingi 2492, hali inayoonesha kupanda kwa bei na kuimarika kwa soko la ufuta.
Kaimu Mwenyekiti wa TAMCU Kaisi Rashid Makolela, amesema kuwa wakulima wote walikubali kuuza kwa bei ya wastani ya soko, kwa kuzingatia sheria na taratibu zinazosimamia minada hiyo. “Ni muhimu mkulima awe na ridhaa ya kuuza mazao yake kwa bei iliyoko mbele yake, na leo tumeona mshikamano mkubwa kutoka kwa wakulima wetu,” alisema Makolela.
Afisa Ushirika, Mkuu Rashid Maengo, amewapongeza wakulima kwa kujitokeza kwa wingi na kuwa mfano wa kuigwa katika ushiriki wa minada ya mazao, amesisitiza kuwa bei nzuri iliyopatikana leo ni matokeo ya ubora wa mazao yaliyokusanywa, na mfumo uliotumika wa TMX umewezesha wanunuzi kutoka maeneo mbalimbali kushiriki mnada bila kuwepo eneo la mnada kwa kutumia njia ya mtandao.
Aidha, amewasihi wakulima kuendelea kuhakikisha taarifa zao binafsi, hasa namba za akaunti, wanazowasilisha kwenye vyama vya msingi, kama ni ni sahihi ili kuepuka ucheleweshaji wa malipo.
Kwa upande wao, wakulima wameeleza furaha yao kwa jinsi mfumo wa TMX unavyorahisisha mauzo na kuwapa uhakika wa malipo kwa wakati, Wameiomba Benki ya Ushirika kupita mara kwa mara katika vijiji ili kuwawezesha kujiunga na huduma za kifedha na kuongeza uzalishaji wa mazao kupitia mikopo.
“Tunashukuru mfumo huu umeturahisishia maisha, tunapata bei nzuri na malipo kwa wakati. Tunaiomba Benki ya ushirika ije vijijini ili na sisi tupate huduma za kibenki na mikopo ya kuendeleza kilimo,”
Kupitia ushirkiano wa wakulima, vyama vya ushirika na serikali, sekta ya kilimo Tunduru inaendelea kuimarika, ikitoa matumaini makubwa kwa wakulima wa ufuta na mazao mengine ya biashara.