Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde,akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa kupokea na kushughulikia kero za wananchi, pamoja na kugawa simu janja kwa wenyeviti wa mitaa 222 wa Jimbo hilo,hafla iliyofanyika leo Juni 26,2025 jijini Dodoma.
Na Alex Sonna,Dodoma
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde, amezindua rasmi mfumo wa kidigitali wa kupokea na kushughulikia kero za wananchi, pamoja na kugawa simu janja kwa wenyeviti wa mitaa 222 wa Jimbo hilo.
Hafla hiyo imefanyika leo Juni 26,2025 jijini Dodoma na kuhudhuriwa na viongozi wa mitaa, wataalamu wa TEHAMA na wananchi mbalimbali.
Akizungumza katika uzinduzi huo, Mavunde amesema mfumo huo wa kipekee unaolenga kurahisisha mawasiliano kati ya wananchi na viongozi wao, ni wa kwanza kutumika katika ngazi ya jimbo nchini Tanzania.
Amesema mfumo huo umejengwa kwa lengo la kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika kushughulikia changamoto za wananchi kwa wakati.
“Kuna nyakati wananchi wamekuwa wakipiga simu kwa mbunge au kiongozi wa mtaa lakini hawampati,Kupitia mfumo huu, taarifa ya mwananchi itawafikia viongozi wote husika kwa wakati mmoja na hii itahakikisha hakuna sauti ya mwananchi inayopotea,” amesema.
Aidha, ameeleza kuwa mfumo huo utatumika katika kata zote 41 za Jimbo la Dodoma Mjini na utakuwa endelevu hata baada ya yeye kuondoka madarakani.
Amesisitiza kuwa Mbunge atakayechukua nafasi yake atapewa mafunzo kuhusu matumizi ya mfumo huo ili aendelee kuwahudumia wananchi kwa viwango vinavyotarajiwa.
Mavunde pia amegawa simu janja kwa wenyeviti wa mitaa 222, akieleza kuwa vifaa hivyo ni nyenzo mahsusi za mawasiliano na ufuatiliaji wa kero, na si anasa.
Amebainisha kuwa simu hizo zimetengenezwa ndani ya nchi, katika kiwanda kilichopo Mkuranga, Pwani, ikiwa ni sehemu ya kuunga mkono uzalishaji wa ndani.
“Simu hizi ni kwa ajili ya kupokea kero za wananchi na kuhakikisha zinatatuliwa,tunaanza ukurasa mpya wa utendaji wa kisasa na wenye uwazi,Viongozi wa mitaa mkivitunza vifaa hivi, mtakuwa mmechochea maendeleo ya kweli kwa jamii,” amesisitiza.
Mavunde ametumia nafasi hiyo pia kuhitimisha rasmi safari yake ya miaka 10 kama Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, akieleza kuwa anaondoka akiwa hana deni kwa wananchi waliompa dhamana.
“Leo ndiyo siku yangu ya mwisho kuwa mbunge wa Dodoma Mjini, Nawashukuru kwa heshima mliyonipa kwa miaka kumi. Mlinipa dhamana, nami niliichukulia kwa uzito. Nimejitahidi kuishi kama mtumishi wa watu, siyo tu kiongozi,” amesema kwa hisia.
Akielezea sababu ya kujitambulisha kama mtumishi wa watu, Mavunde amesema uzoefu wake katika kukutana na wananchi waliokuwa na changamoto mbalimbali, hasa katika mazingira ya misiba, ulimfanya kuchukua hatua kubwa.
Alikumbusha namna alivyokutana na mwananchi aliyebeba maiti kwenye pikipiki, jambo lililomgusa sana na kumfanya aagize gari maalum kwa ajili ya kusaidia usafirishaji wa miili ya wapendwa wa wananchi wake.
“Nilitukanwa sana, lakini sikutishika. Nilichagua kuwa sehemu ya suluhisho badala ya kuchangia laki tatu kila siku. Hii ndiyo maana ya kweli ya utumishi,” alieleza huku akipaza sauti ya ujasiri.
Katika kuhitimisha, Mavunde ametangaza kuchangia shilingi milioni 10 kwa ajili ya kuanzisha SACCOs ya wenyeviti wa mitaa wa Dodoma Mjini ili kuwaimarisha kiuchumi na kuongeza nguvu ya uongozi wa msingi.
“Siku zote tutakuwa pamoja, tutatenganishwa tu na mipaka ya kijiografia, lakini moyo wangu utaendelea kuwa na wananchi wa Dodoma Mjini,” alisema kwa hisia nzito.
Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde,akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa kupokea na kushughulikia kero za wananchi, pamoja na kugawa simu janja kwa wenyeviti wa mitaa 222 wa Jimbo hilo,hafla iliyofanyika leo Juni 26,2025 jijini Dodoma.
Sehemu ya washiriki wakimsikiliza Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini na Waziri wa Madini, Mhe. Anthony Mavunde (hayupo pichani) wakati wa hafla ya uzinduzi wa mfumo wa kidigitali wa kupokea na kushughulikia kero za wananchi, pamoja na kugawa simu janja kwa wenyeviti wa mitaa 222 wa Jimbo hilo,hafla iliyofanyika leo Juni 26,2025 jijini Dodoma.