Mkoa wa Iringa, Tanzania,
Serikali kupitia Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imeanza rasmi utekelezaji wa mradi mkubwa wa ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umwagiliaji, mradi unaolenga kuleta mageuzi ya uzalishaji kwa zaidi ya wakulima 8,600 katika Kata ya Ilolompya, wilayani Iringa.
Mradi huu, unaogharimu takriban Shilingi bilioni 33.8, ni sehemu ya juhudi za serikali kuongeza tija ya kilimo na kuhakikisha wakulima wanalima misimu yote miwili kwa ufanisi zaidi bila kutegemea mvua zisizotabirika.
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mradi huo, Mhandisi wa Umwagiliaji wa mkoa wa Iringa, Peter Akonaay, alisema utekelezaji huo unahusisha ujenzi mpya na ukarabati wa skimu kwenye jumla ya ekari 20,250, huku maeneo ya Luganga, Magozi, Ukwega, Ilolompya na Mkombilenga yakiwa miongoni mwa yanayofaidika.
“Mradi huu utaboresha maisha ya wakulima kupitia kilimo chenye tija, huku kaya 2,276 zikinufaika moja kwa moja,” alisema Mhandisi Akonaay, akibainisha kuwa mradi unatarajiwa kukamilika ndani ya mwaka mmoja.
Skimu ya Magozi peke yake itajumuisha ekari 3,250 zenye miundombinu ya kisasa, huku Luganga ikiongeza uwezo wa umwagiliaji hadi ekari 1,700. Mazao yanayotarajiwa kulimwa ni pamoja na mpunga, mahindi, mihogo, nyanya, maharagwe na mbogamboga.
Wananchi wa maeneo husika, hususan kutoka Tarafa ya Pawaga, wamepongeza hatua hiyo wakieleza kuwa ni suluhisho la muda mrefu dhidi ya utegemezi wa mvua.
“Ni ukombozi mkubwa kwa sisi wakulima. Tutakuwa na uhakika wa chakula na kipato mwaka mzima,” alisema mmoja wa wakazi wa Ukwega.
Tume ya Taifa ya Umwagiliaji imesisitiza kuwa jamii itashirikishwa kikamilifu katika utekelezaji wa mradi huo, huku mafunzo ya matumizi bora ya maji na mbinu za kilimo bora yakitolewa ili kuhakikisha uendelevu wa miundombinu hiyo.
Mradi huu ni miongoni mwa miradi ya kimkakati inayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2024/2025, na unatekelezwa na Kampuni ya CREC (EA) Ltd.