Na Mwamvua Mwinyi-Pwani
Juni 26, 2025 – Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, Nsajigwa George, ametoa rai kwa asasi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) kufanya kazi kwa kuzingatia kanuni, taratibu, uwazi na uwajibikaji ili kuongeza ufanisi na mchango wao kwa jamii.
Nsajigwa alitoa wito huo ,wakati akifungua Mkutano wa Jukwaa la Mashirika Yasiyo ya Kiserikali Mkoa wa Pwani, uliofanyika katika Ukumbi wa Resosi, Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Pwani, Kibaha.
Amesisitiza kuwa ni muhimu kwa mashirika hayo kuzingatia misingi ya kisheria katika utekelezaji wa majukumu yao, huku akionya dhidi ya kutoa taarifa au kufanya shughuli zinazoweza kuibua taharuki, hasa katika kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
“Mwaka 2025 ni mwaka wa uchaguzi,Napenda kusisitiza kuwa mashirika yote yafanye kazi kwa kuzingatia sheria na kanuni,Msijihusishe na migawanyiko ya kisiasa wala kuchochea taharuki”
“Tunawategemea katika kulinda amani na utulivu, ambavyo ni tunu ya taifa letu,Kila mmoja ana jukumu la kuilinda,” alisema Nsajigwa.
Aidha, alibainisha mashirika yasiyo ya kiserikali ni wadau muhimu wa serikali katika kusukuma mbele maendeleo ya kijamii na kiuchumi, hivyo ni lazima yawe mfano wa kuigwa katika kuimarisha mshikamano, amani na maendeleo endelevu.