Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akizungumza wakati akihitimisha mjadala wa Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na viongozi Wakuu Wastaafu kuhusu “Maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za Afrika na Caribbean” katika Mkutano wa 32 wa Benki ya Afrexim unaofanyika Abuja nchini Nigeria leo tarehe 27 Juni 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki katika Mkutano wa 32 wa Benki ya Afrexim unaofanyika Abuja nchini Nigeria leo tarehe 27 Juni 2025.
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango akishiriki uzinduzi wa kadi ya kielekroniki ya malipo ya pamoja ya nchi za Afrika wakati wa Mkutano wa 32 wa Benki ya Afrexim unaofanyika Abuja nchini Nigeria leo tarehe 27 Juni 2025.
………………….
Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Philip Mpango amesema migogoro ya kimataifa inapaswa kuwa funzo kwa nchi za Afrika namna ya kuendelea kushirikiana zaidi ikiwemo kutekeleza miradi ya kikanda kama vile ya usafirishaji na miundombinu ili kuunganisha bara hilo.
Makamu wa Rais amesema hayo wakati akihitimisha mjadala wa Wakuu wa Nchi na Serikali pamoja na viongozi Wakuu Wastaafu kuhusu “Maendeleo ya kiuchumi kwa nchi za Afrika na Caribbean” uliofanyika katika Mkutano wa 32 wa Benki ya Afrexim unaofanyika Abuja nchini Nigeria.
Amesisitiza umuhimu wa Bara la Afrika kujenga uchumi imara na himilivu kwa kuwa uchumi wa dunia unakabiliwa na misukosuko mbalimbali.
Makamu wa Rais amesema ni vema kudhibiti mfumuko wa bei za vyakula, kuangazia usalama wa chakula na kupunguza uagizaji kutoka nje ya Bara la Afrika. Pia ameongeza kwamba, kwa kuwa sekta ya nishati ni nguzo katika maendeleo ya kiuchumi ni vema nchi za Afrika kushirikiana kuhakikisha mfumuko wa bei katika nishati unadhibitiwa.
Halikadhalika, Makamu wa Rais amesema ni vema kuwekeza katika nguvu kazi ya vijana ikiwemo kuwandaa na kuwapa uongozi kwa maendeleo ya Bara la Afrika.
Mkutano wa 32 Benki ya Afrexim unawakutanisha zaidi ya washiriki 6000 ikiwemo Wakuu wa Nchi na Serikali, Mawaziri, Magavana wa Benki, Wadau pamoja na wananchi mbalimbali.
Benki ya Afrexim ilianzishwa mwaka 1993, mahususi kwaajili ya kutoa mikopo kwa wafanyabiashara na wajasiriliamali mbalimbali wa Afrika pamoja na ufadhili wa miradi mbalimbali ya maendeleo barani Afrika.