WAKULIMA wa Zabibu Kata ya Mpunguzi, Jijini Dodoma wameeleza kunufaika na Kilimo cha zabibu kutokana na kuongezeka kwa tija wanayoipata katika mnyororo mzima wa thamani wa zao hilo la kibiashara ambalo wanasema upatikanaji wa soko la bidhaa zake zilizoongezewa thamani ni mkubwa.
Hayo yamesemwa Leo Juni 26, 2025 na Mwenyekiti wa Umoja wa Wakulima wa Zabibu na Masoko Mpunguzi (UWAZAMAM) Bwana, Moses Masasi katika mafunzo kwa Wakulima wa Zabibu yanayotolewa kwa siku mbili na Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania (TARI) kupitia kituo cha TARI Makutupora yakiwa na lengo la kuongeza tija katika uzalishaji wa zao hilo.
Akieleza hilo, Masasi anasema kabla hawajapata mafunzo kutoka TARI walikuwa wakizalisha wastani wa tani Moja na nusu kwa Ekari lakni baada ya kupata mafunzo kutoka kwa Watafiti wanazalisha wastani wa tani nne Hadi sita kwa Ekari.
Pia amesema tija nyingine ni katika usindikaji ambapo anasema kutokana na uhakika wa uzalishaji kuongezeka ambao ni matokeo ya Mafunzo ambayo wamekuwa wakipata kutoka TARI Makutupora kupitia Umoja wa UWAZAMAM wanajihusisha na uongezaji thamani wa zao hilo katika upande wa usindikaji wa mvinyo na kupata uhakika wa soko ambao ni mkubwa na inawapa tija zaidi.
Kwa upande wake Mtafiti Mwandamizi kutoka kituo cha TARI Makutupora Bi. Dainess Sanga amesema lengo la mafunzo hayo ni kufundisha kanuni bora za Kilimo cha Zabibu ili kuongeza tija zaidi kwa Wakulima katika mnyororo wa thamani wa zao hilo.
