Na mwandishi wetu, Kiteto
MBUNGE wa Jimbo la Kiteto Mkoani Manyara, anayemaliza muda wake wakili msomi Mhe Edward Ole Lekaita Kisau amesema wananchi wa Kiteto, wamenufaika na miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwemo ya sekta ya afya, miundombinu, elimu, maji na mingineyo kwa muda wa miaka mitano ya 2020/2025 iliyogharimu kiasi cha fedha cha shilingi bilioni 156,413,695,240.10.
Ole Lekaita ameyaelezea hayo kupitia taarifa yake kwa vyombo vya habari iliyosheheni miradi ya maendeleo mbalimbali yaliyofanyika kwa kipindi chake cha uongozi wa miaka mitano 2020/2025.
Ole Lekaita ameeleza kwamba wananchi wa Kiteto wamenufaika na miradi hiyo ya maendeleo ya zaidi ya Sh156.4 bilioni iliyofanyika kwa muda wa miaka mitano kupitia ahadi mbalimbali walizopatiwa wakati wa kampeni mwaka 2020.
“Kwa furaha kubwa napenda kuwafahamisha wananchi wenzangu wa Kiteto kuwa ndani ya miaka mitano zaidi ya Sh156.4 bilioni ni fedha za miradi yote iliyotekelezwa kwenye jimbo letu,” amesema Ole Lekaita.
Amesema kata zote 23 za jimbo la Kiteto zimenufaika na fedha hizo kupitia miradi ya maji, miundombinu ya barabara, nishati ya umeme, ujenzi wa madarasa ya shule shikizi, za msingi na sekondari, nyumba za walimu, mabweni, mabwalo, ofisi, zahanati na vituo vya afya.
“Nawashukuru wananchi wa Kiteto kwa ushirikiano walionipa, naishukuru serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan, nakishukuru chama changu CCM kwa kunipa ridhaa ya kupeperusha bendera na wadau wote wa maendeleo,” amesema Ole Lekaita.
Hata hivyo, ameeleza kwamba kwa upande wa migogoro ya ardhi, awali, baadhi ya wakulima walikuwa wanalalamikia mifugo kuingizwa mashambani mwao na kupigwa na baadhi ya wafugaji.
Amesema baadhi ya wafugaji pia nao walilalamikia kuwa baadhi ya wakulima wanalima maeneo ya mifugo na mifugo kujeruhiwa kwa kukatwa katwa na wakulima wanapokutwa mashambani.
Amesema hali hiyo ilileta changamoto kubwa na kuibua hisia mseto katika jamii, kuleta ubaguzi na kusababisha mahusiano mabovu baina ya wakulima na wafugaji.
“Mtakumbuka kuwa mahusiano kati ya wakulima na wafugaji yalikuwa mabaya sana, ila hivi sasa wanaishi pamoja kama ndugu kwani wote wanategemeana,” amesema Ole Lekaita.
Amesema kwenye uchaguzi wa mwaka 2020 wana Kiteto waliamua kumchagua mwakilishi wao atakayewaunganisha bila ubaguzi na kukomesha mgogoro wa wakulima na wafugaji kwani walichoshwa na kutaka amani na mshikamano.
Ametaja baadhi ya changamoto zilizobaki ni miundombinu ya barabara kuu kubwa mbili za lami ya Kongwa-Kiteto-Simanjiro-Arusha ya kilomita 450 na barabara ya Tanga-Handeni-Kibirash-Kiteto-Chemba-Singida ya kilomita 460.
“Wana Kiteto wanakumbuka kuwa nimezungumza mara nyingi ndani ya bunge la 12 kuelezea juu ya umuhimu wa ujenzi wa barabara kuu mbili za lami kwa maendeleo ya jimbo letu,” amesema Ole Lekaita.
Mkazi wa kata ya Sunya Kulwa Mkamba ameeleza kwamba maendeleo yaliyopatikana kwa muda wa miaka mitano ya ubunge wa Ole Lekaita ni historia kwa jimbo la Kiteto.
“Kwa kipindi cha miaka mitano aliyoongoza Ole Lekaita wana Kiteto wameona maendeleo yaliyofanyika kwa muda mfupi hivyo katika kata zetu zote hii ni historia mpya kwake na wana Kiteto tumeona na tutamlipa,” amesema Mkamba.