Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Carolyne Nombo,akiwaongoza Watumishi wa Wizara hiyo kumpokea Naibu Katibu Mkuu Mpya Wizara hiyo ,anayeshughulikia Elimu Dkt.Hussen Mohamed Omar,akisalimiana na watumishi mara baada ya kuwasili katika ofisi za Wizara hiyo leo Juni 27,2025 Mtumba Jijini Dodoma.
Na.Alex Sonna-DODOMA
NAIBU Katibu Mkuu Mpya Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia,anayeshughulikia Elimu Dkt.Hussen Mohamed Omar leo Juni 27,2025 amepokelewa rasmi wizarani hapo huku akiahidi ushirikiano kwa watumishi wenzake ili kuweze kutekelezaji majukumu.
Dkt.Omar ametoa ahadi hiyo mara baada ya kupokelewa na Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu,Sayansi na Teknolojia Prof.Carolyne Nombo pamoja na watumishi katika ofisi za Wizara hiyo Mtumba Jijini Dodoma.
Aidha Dkt.Omar,ametoa shukrani kwa mapokezi mazuri aliyoyapata kutoka kwa watumishi wa wizara huku akisisitiza kuwa yupo tayari kuwajibika ipasavyo katika kuendeleza mageuzi ya Elimu katika nyanja zote.
“Namshukuru Mheshimiwa Rais kwa kuendelea kuniamini na kuona kuwa huduma yangu bado inahitajika,niahidi kuwa nitajifunza mengi kutoka kwenu kutokana kuwa ofisi hii ina walimu wengi,pia nitatoa ushirikiano wa kutosha maana na mimi naamini kufanya kazi kwa ushirikiano,”amesema Dkt.Omar
Aidha Dkt.Omar amehamishwa kutoka Wizara ya kilimo kwenda Wizara ya Elimu kuchukua nafasi ya aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Dkt. Wilson Charles Mahera ambaye anaenda kutia nia ya kugombea ubunge katika Jimbo la Butiama mkoani Mara.
Awali Katika hotuba yake ya kumkaribisha Katibu Mkuu wa Wizara hiyo Prof.Carolyne Nombo,amesema kuwa Wizara inaendelea kutekeleza mageuzi makubwa ya elimu yanayolenga kutoa stadi,maarifa na ujuzi kwa watanzania.
“Naamini kuwa tutakwenda kujifunza mambo mengi,tutaonesha ushirikiano mkubwa kutoka kwako Dkt.Omar,Wizara hii tumejipanga kutekeleza vitu vingi ikiwemo sera mpya ya masomo na tunayo mitaala iliyo boreshwa,Wizara yetu inafanya kazi kwa kushirikiana na TAMISEMI na taasisi nyingine hivyo tupo tayari kukupa ushirikiano kama na wewe ulivyo tuahidi,”amesema Prof. Nombo
Pia Prof.Nombo amemshukuru aliyekuwa Naibu katibu Mkuu Dkt.Wilson Mahera kwa kazi nzuri aliyoifanya katika kipindi chote hicho huku akimtakia kila la heri huko aendako.
Naye aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu Wizara hiyo Dkt. Wilson Charles Mahera, amemshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe.Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kumuamini katika kazi kwa kipindi chote cha utawala wake ambapo alimteua kuhudumu nafasi tofauti katika Wizara mbalimbali.