

WANARIADHA mahiri John Joseph na Tunu Andrea wameibuka washindi wa kwanza katika Mbio za Nusu Marathon (km 21) kwa upande wa wanaume na wanawake, na kujinyakulia zawadi ya shilingi milioni moja (1,000,000/-) kila mmoja katika Mbio za Kimataifa za Utalii Kanda ya Ziwa (Lake Zone International Tourism Marathon 2025), zilizofanyika kwa lengo la kuhamasisha afya ya mama na mtoto.
Katika mbio za kilomita 10, Naomi Mwarija aliibuka mshindi kwa upande wa wanawake huku Emmanuel Joseph akishika nafasi ya kwanza kwa wanaume. Kila mmoja alizawadiwa shilingi 700,000. Mbio hizo pia zilihusisha kundi la wanawake wajawazito zaidi ya 300 waliotembea umbali wa kilomita 2.5 kama sehemu ya kuhamasisha mazoezi kwa afya bora.
Akizungumza leo wakati wa hafla ya kukabidhi zawadi kwa washindi, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dkt. Jesca Lebba alisema mbio hizo zimelenga kusaidia ununuzi wa vifaa vya uzazi pamoja na kuelimisha jamii juu ya uzazi salama yakiwemo magonjwa yasiyoambukiza.
“Michezo ni afya na pia ni uchumi. Afya ni mtaji wa maisha ya binadamu,wajawazito wanapofanya mazoezi huongeza uwezekano wa kujifungua salama, hupunguza msongo wa mawazo, huongeza uwezo wa kufikiri na kusaidia kujenga kinga dhidi ya magonjwa yasiyoambukiza,” alisema Dkt. Lebba.
Alipongeza ushiriki wa sekta binafsi, hususan Kampuni ya Kilimanjaro One Sports Promotion Ltd, kwa kuandaa mashindano hayo yenye lengo la kuboresha huduma za afya, na kuongeza kuwa juhudi hizo zinaiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, ambaye kupitia filamu ya Royal Tour ameongeza mwamko wa utalii nchini, ikiwemo Kanda ya Ziwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Kilimanjaro One Sports Promotion Ltd, Mohamed Khatibu alisema mashindano hayo yameanzishwa kwa mara ya kwanza Kanda ya Ziwa, yakilenga kusaidia sekta ya afya, hasa huduma kwa wajawazito na watoto.
“Tumelenga kusaidia upatikanaji wa vifaa vya uzazi na kuhamasisha mazoezi kwa wajawazito. Lengo ni kuhakikisha vifaa hivyo vinawafikia walengwa katika vituo vya afya, na kusaidia kupunguza changamoto wanazokutana nazo wakati wa kujifungua,” alisema Khatibu.
Aliongeza kuwa kutokana na mafanikio waliyoyapata, wanatarajia kupanua mashindano hayo ama kuongeza maeneo mengine yenye mahitaji makubwa ya huduma za afya kwa mama na mtoto.
Baadhi ya wajawazito walioshiriki mbio hizo, akiwemo Pracidia Philimon na Marina Mathias, waliishukuru kampuni hiyo kwa kuandaa tukio hilo, wakisema mazoezi huimarisha nyonga na kusaidia kujifungua bila upasuaji.
“Wajawazito wengi tumekuwa tukisumbuliwa na maumivu ya nyonga kwa sababu ya kutofanya mazoezi. Mbio hizi ni suluhisho. Tumejifunza kuwa hata kutembea kilomita moja au mbili kuna faida kubwa,” alisema Pracidia.
Naye Marina alisema: “Mazoezi ni tiba. Mbio hizi ni fursa ya pekee, zinatusaidia kuimarisha afya na kuepuka upasuaji. Tunawashukuru sana Kilimanjaro One Sports.”
Kwa upande wake, mshindi wa mbio za km 21 kwa wanaume, John Joseph, aliwapongeza wajawazito waliothubutu kushiriki mbio hizo, na kuwataka wanawake wajawazito wengine kutambua umuhimu wa mazoezi kwa ustawi wa afya yao na watoto wao