NA DENISMLOWE, IRINGA.
DAKTARI Musa Mdede kwa mara nyingine tena baada ya mwaka 2020 kuchukua fomu na kushika nafasi ya nne amejitokeza tena mwaka huu kuomba ridhaa ya wana Ccm jimbo la Kalenga awe mwakilishi wao katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu.
Musa Mdede amechukua rasmi fomu ya kugombea Ubunge wa Jimbo la Kalenga majira ya saa nne asubuhi mbele ya waandishi wa habari na kusema kuwa yuko tayari kwa ajili ya kupambana katika kura za maoni endapo jina lake litapitishwa.
Akizungumza mara baada ya kuchukua fomu Dr. Mdede aliishukuru CCM kwa kuendelea kutoa nafasi kwa makada wake hususan vijana,m kushiriki kikamilifu katika nafasi za uongozi kuelekea uchaguzi Mkuu.
Aidha Dr. Mdede alipongeza Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kwa mafanikio makubwa yaliyopatikana katika sekta mbalimbali akisema yameongeza matumaini na hamasa katika kuijenga nchi.
Alibainisha kuwa atatoa maelezo zaidi kuhusu dira na mikakati yake endapo chama kitampa ridhaa ya kuendelea na safari ya kugombea ubunge.
Dr. Mdede ni mkazi wa Kata ya Nzihi akiwa na umri wa miaka 37 ni daktari kwa taaluma na mhitimu wa Shahada ya Udaktari wa Binadamu (MD) akiwa na uzoefu mkubwa wa uongozi tangu akiwa mwanafunzi chuoni ambapo mwaka 2013/14 alikuwa Rais wa Serikali ya Wanafunzi wa CUHAS-Bugando na pia aliongoza jumuiya ya wanafunzi wa vyuo vikuu kupitia TAHLISO.
Alikuwa pia mjumbe wa Baraza la TCU na TACUSU mwaka huo na katika siasa Dr. Mdede aligombea Ubunge wa Kalenga mwaka 2015 kupitia CHADEMA na kushika nafasi ya pili nyuma ya mgombea wa CCM.
Mwaka 2020 alirejea CCM na kushika nafasi ya nne kati ya wagombea 67 waliowania kupitishwa kugombea jimbo hilo na Kwa sasa ni mjumbe wa Mkutano Mkuu wa CCM Mkoa wa Iringa, Halmashauri Kuu ya CCM Wilaya ya Iringa Vijijini, na Kamati ya UVCCM ya Elimu na Propaganda Mkoa wa Mbeya.


