Na. Mwandishi wetu, Katavi.
Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira vijijini (RUWASA) wilaya ya Tanganyika wamekamilisha mradi wa maji wa kisima chenye urefu wa mita 120 chenye uwezo wa kuzalisha maji zaidi ya lita 6,000 kwa saa; kilichogharimu kiasi cha shilingi milioni 101.
Mradi huo upo katika kijiji cha Isubangala katika halmashauri ya wilaya ya Tanganyika mkoani Katavi; ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa mradi wa visima 900; hali iliyopelekea kuwanufaisha zaidi ya wakazi 1,800 wa kijiji hicho.
Katika wilaya ya Tanganyika visima hivyo vimechimbwa vitano katika vijiji vya Isubangala, Mgansa, Kusi, Busongola na Bugwe.
Wakizungumzia manufaa ya mradi huo wakazi wa kijiji hicho akiwemo Pendo Laban wamesema wameondoa adha ya kutembea umbali mrefu kutafuta maji katika mito na visima vya kienyeji.
Akitoa taarifa ya mradi huo Mhandisi Msimamizi wa mradi huo kutoka RUWASA Eng. Belius Emmanuel amesema mradi huo umekamilika na umeanza kutumika.
Akizungumza mara baada ya kuzindua mradi huo mkuu wa wilaya ya Tanganyika Onesmo Buswelu amewataka wananchi kuutunza mradi huo.
Aliongeza kuwa serikali imekuwa ikiboresha huduma mbalimbali za wananchi ili kupunguza changamoto zilizopo katika jamii.