Na Mwandishi Wetu – Dar es Salaam
Katika kuimarisha ushirikishwaji wa wananchi kwenye masuala ya ulipaji kodi na kukuza uelewa kuhusu haki na wajibu wa mlipakodi, Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) imeendelea kusogeza huduma zake kwa wananchi kupitia banda lake katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF) yanayoendelea katika viwanja vya Sabasaba, Barabara ya Kilwa.
Akizungumza na waandishi wa habari Juni 30, 2025, Mkurugenzi wa Elimu kwa Mlipa Kodi na Mawasiliano wa TRA, Richard Kayombo alisema mamlaka hiyo imeshiriki maonesho hayo kwa lengo la kutoa huduma za moja kwa moja na elimu ya kina kwa wananchi na wafanyabiashara.
“Tumekuja hapa si tu kwa ajili ya kutoa TIN namba bali pia kuwaelimisha wananchi kuhusu masuala mapya na ya msingi kwenye ulipaji kodi, ikiwemo vivutio vya kodi kwa sekta za kilimo, namna ya kuagiza bidhaa kutoka nje, na bidhaa zinazofaidika na misamaha ya kodi,” amesema Kayombo.
Kayombo amesema kuwa kwa mara nyingine, TRA inatumia Sabasaba kama jukwaa la karibu zaidi kati ya mamlaka na walipa kodi, ambapo wananchi wanaweza kupata huduma kama usajili wa TIN, elimu juu ya stempu za kodi, utambuzi wa bidhaa bandia, pamoja na huduma za ushauri kuhusu kodi za biashara na za mtu binafsi.
Mbali na huduma hizo, wananchi pia wanaelimishwa kuhusu njia sahihi za kutoa taarifa dhidi ya wafanyakazi wa TRA wasio waaminifu au wenye mwenendo usio wa kimaadili, huku mamlaka ikieleza wazi hatua zinazochukuliwa dhidi ya watumishi hao.
“Tunawahimiza wananchi kutokuwa waoga, wajitokeze kuripoti ukiukwaji wa maadili kwani tunachukua hatua kali kwa mujibu wa taratibu. Tupo hapa kusikiliza na kutoa msaada wa papo kwa papo,” ameongeza.
Banda hilo pia linawapa fursa wananchi kufahamu bidhaa zinazopaswa kuwa na stempu za kodi (electronic tax stamps) na athari za matumizi ya bidhaa bandia, ikiwa ni sehemu ya mkakati wa kulinda afya ya walaji na mapato ya Serikali.
Kwa ujumla, ushiriki wa TRA katika maonesho haya si tu kusogeza huduma, bali ni sehemu ya mpango mpana wa kujenga utamaduni wa ulipaji kodi kwa hiari, maadili katika biashara na uwajibikaji kwa maendeleo ya Taifa.