Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Daniel Mushi, leo tarehe 1 Julai 2025, amekutana na uongozi mpya wa Wamiliki wa Shule na Vyuo Binafsi Tanzania (TAMONGSCO), katika ofisi za Wizara hiyo jijini Dodoma.
Uongozi huo umefika kujitambulisha rasmi baada ya kuchaguliwa upya, na pia kuonesha dhamira ya kushirikiana na Serikali katika kuboresha sekta ya elimu nchini.
Akizungumza katika kikao hicho, Prof. Mushi amesisitiza kuwa Serikali inaweka mkazo katika ushirikiano na wadau mbalimbali wa elimu, ili kuhakikisha utekelezaji wa mageuzi ya elimu unaleta matokeo chanya ili kuwawezesha vijana kupata maarifa, stadi na ujuzi unaowawezesha kushindana katika soko la ajira, na hivyo kuchangia kikamilifu katika maendeleo ya Taifa.
Kwa upande wake, Makamu Mwenyekiti wa TAMONGSCO Taifa, Bw. Mathew Levi Alex, amesema uongozi wao umejipanga vyema kutekeleza Sera ya Elimu kwa vitendo, ikiwa ni pamoja na kuwekeza katika miundombinu ya elimu ya Amali ambayo Serikali imeipa kipaumbele kikubwa.
βΒ