Na Mwandishi Wetu, Babati
Babati, Juni 30, 2025 — Aliyekuwa Mhasibu Msaidizi wa Kituo cha Afya Endagwe wilayani Babati, Mohamed Twalib Baya, amefikishwa katika Mahakama ya Wilaya ya Babati, Mkoa wa Manyara, kujibu mashtaka ya rushwa, uhujumu uchumi na kughushi nyaraka.
Shauri hilo la Uhujumu Uchumi lenye namba 15921/2025 limesikilizwa mbele ya Hakimu Mkazi Mwandamizi Mheshimiwa Martin Masao, ambapo mshtakiwa alisomewa mashtaka yanayomkabili na kuamriwa kubakia mahabusu baada ya kushindwa kukidhi masharti ya dhamana.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka iliyosomwa na Mawakili wa Serikali kutoka TAKUKURU Bi. Neema Gembe, Bw. Davis Masambu na Bi. Catherine Ngessy, mshtakiwa anadaiwa kufanya ubadhirifu wa fedha kiasi cha Shilingi milioni 8.015, kinyume na Kifungu cha 28(1) cha Sheria ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sura ya 329 kama ilivyofanyiwa marejeo mwaka 2022.
Aidha, anadaiwa kuisababishia Serikali hasara kinyume na Aya ya 10(1) ya Jedwali la Kwanza pamoja na vifungu vya 57(1) na 60(2) vya Sheria ya Uhujumu Uchumi na Makosa ya Kupangwa, Sura ya 200 marejeo ya 2022. Mbali na makosa hayo, mshtakiwa pia anakabiliwa na tuhuma za kughushi nyaraka kinyume na vifungu vya 333, 335(a) na 337 vya Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Sura ya 16 marejeo ya mwaka 2022.
Mshtakiwa Mohamed Baya amekana mashtaka yote yanayomkabili. Kesi imeahirishwa hadi Julai 1, 2025 kwa ajili ya uamuzi juu ya dhamana, huku mshtakiwa akiendelea kushikiliwa mahabusu.