Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisalimiana na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, alipowasili kwa ajili ya kuhudhuria katika kikao cha wafanyakazi wa Wizara yake kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akisalimiana na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Christian Omolo, alipowasili kwa ajili ya kuhudhuria katika kikao cha wafanyakazi wa Wizara yake kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba. Anayeshuhudia ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha- Usimamizi wa Fedha za Umma, Bi. Amina Shaaban (kulia).
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akizungumza na Watumishi wa Wizara ya Fedha, wakati wa kikao cha watumishi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba. katika ukumbi wa Jiji Mtumba, ambacho kilitoa fursa kwa watumishi kukutana kwa pamoja, kukumbushana na kubadilishana uzoefu, taarifa na uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Serikali kwa ujumla.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiteta jambo na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, wakati wa kikao cha watumishi kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba, ambacho kilitoa fursa kwa watumishi kukutana kwa pamoja, kukumbushana na kubadilishana uzoefu, taarifa na uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Serikali kwa ujumla.
Watumishi wa Wizara ya Fedha, wakifuatilia hotuba ya Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (hayupo pichani), wakati akizungumza na Watumishi wa Wizara hiyo, katika Kikao cha Watumishi, kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba.
Waziri wa Fedha Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Wizara hiyo wakati wa Kikao cha Watumishi wa Wizara hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba. Kushoto kwake ni Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El- maamry Mwamba, akifuatiwa na Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Christian Omolo na Mkaguzi wa Ndani Mkuu wa Serikali (IAG), Bw. Benjamin Magai. Kulia ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha- Usimamizi wa Fedha za Umma, Bi. Amina Shaaban, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Usimamizi wa Uchumi, Bw. Elijah Mwandumbya, Mhasibu Mkuu wa Serikali CPA (T), Leonard Mkude.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), akiteta jambo na Mhasibu Mkuu wa Serikali CPA (T), Leonard Mkude, baada ya kumalizika kwa Kikao cha Watumishi wa Wizara hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba.
Meza Kuu ikiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali Dkt. Natu El- maamry Mwamba, wakiwa katika picha ya pamoja na viongozi wa Menejimenti ya Wizara ya Fedha, baada ya kumalizika kwa Kikao cha Watumishi wa Wizara hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba.
Mchumi Mkuu Wizara ya Fedha, Bw. Mudith Cheyo, akichangia mada wakati wa majadiliano ya Kikao cha Watumishi wa Wizara hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba, kwa ajili ya kushauriana na kubadilishana uzoefu juu ya masuala mbalimbali yanayohusu Wizara, Taasisi na Serikali kwa ujumla.
Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha-Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Christian Omolo, akiperuzi Jarida la Hazina Yetu Toleo la Tatu, wakati wa Kikao cha Watumishi wa Wizara hiyo kilichofanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba. (Picha na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, WF, Dodoma)
……………
Na. Farida Ramadhani, WF, Dodoma.
Waziri wa Fedha, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb), amewaagiza viongozi na watumishi wa Wizara hiyo kuendelea kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu ili kuendelea kusimamia uchumi wa nchi.
Ametoa agizo hilo katika Ukumbi wa Mikutano wa Jiji la Dodoma uliopo Mji wa Serikali, Mtumba, wakati wa Kikao cha watumishi wa Wizara hiyo ambacho kinatoa fursa kwa watumishi kukutana kwa pamoja, kukumbushana na kubadilishana uzoefu, taarifa na uelewa kuhusu masuala mbalimbali yanayohusu utekelezaji wa majukumu ya Wizara na Serikali kwa ujumla.
Dkt. Nchemba aliwakumbusha watumishi hao kutambua kuwa Wizara ya Fedha ni moyo wa Serikali hivyo ikiyumba tu nchi itayumba na kuleta madhara kijamii na kiuchumi.
Aliwasisitiza waendelee kufanya kazi kwa umoja na ushirikiano pamoja na kufanya marekebisho katika maeneo yenye changamoto ili kuboresha utendaji wao na kufikia malengo yaliyowekwa.
”Tutumie kikao hiki kurekebisha maeneo yote yenye changamoto, hakuna binadamu aliyekamilika na ukijiona mkamilifu ujue unamkufuru Mwenyezi Mungu, hivyo inabidi tukubali kubadilika ili kuboresha utendaji wetu”, Alisisitiza Dkt. Nchemba.
Aidha, aliwapongeza watumishi hao kwa kufanya kazi kwa weledi na kuiwezesha nchi kuendelea kutekeleza miradi ya maendeleo na kuhimili changamoto mbalimbali za kiuchumi zinazoendelea ulimwenguni.
’’Mmekuwa mstari wa mbele kuliwezesha Taifa kuhimili misukusuko ya kiuchumi chini ya uongozi madhubuti wa Mhe. Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan, utekelezaji wa miradi ya maendeleo na usimamizi imara wa uchumi unaendelea licha ya misukosuko inayoendelea duniani’’, alibainisha Dkt. Nchemba.
Aliongeza kuwa utendaji wa watumishi wa Wizara hiyo umeiwezesha nchi kutekeleza miradi ya maendeleo lakini pia kuwaongezea sifa binafsi Waziri na Naibu wake Mhe. Hamad Hassan Chande (Mb).
Dkt. Nchemba alisema Serikali itaendelea kuwajengea uwezo watumishi ili waweze kufanya vizuri zaidi katika majukumu yao na kuiwezesha nchi kufikia malengo yake.
Kwa upande wake, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mlipaji Mkuu wa Serikali, Dkt. Natu El-maamry Mwamba, aliwaasa Watumishi wa Wizara hiyo kuongeza ufanisi katika usimamizi wa mapato na matumizi ya mali na fedha za umma ili kufikia malengo ya Serikali katika mwaka wa fedha 2025/26.
Alisema ni muhimu kwa watumishi hao kutumia weledi na uzoefu walionao kuongeza tija katika usimamizi wa sera, sheria, kanuni na miongozo ya masuala ya fedha na bajeti ili kuwezesha Wizara kutekeleza kwa ufanisi malengo yake na Serikali kwa ujumla.
”Ninapenda kuwakumbusha watumishi wote kutekeleza majukumu yetu kwa kuzingatia malengo, shabaha na mpango na bajeti iliyoidhinishwa na Bunge pamoja na kutunza siri na kuhifadhi nyaraka muhimu za Wizara na Serikali kwa ujumla”, alisisitiza Dkt. Mwamba.
Aliwataka Wakuu wa Idara/Vitengo pamoja na watumishi wote kuzingatia maelekezo hayo kwa ukamilifu katika utekelezaji wa majukumu yao.
Naye Naibu Katibu Mkuu anayesimamia Huduma za Hazina, Bi. Jenifa Christian Omolo alisisitiza umuhimu wa kufanyakazi kwa upendo, umoja na mshikamano pamoja na kuendelea kusimamia maadili ya kazi ili kuwezesha wote kufikia malengo yao.
”Wote tunategemeana hakuna mtu anayejua kila kitu, hivyo ni muhimu kupeana nafasi ya kuweza kufikia mafanikio yetu, hakuna mtu anayeweza kufanikiwa bila kuwezeshwa”, alisisitiza Bi. Omolo.
Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha, Usimamizi wa Uchumi, Bw. Elijah Mwandumbya, aliwapongeza watumishi wa Wizara hiyo kwa ushirikiano wao katika utekelezaji wa majukumu yao.
Alisema watumishi wamekuwa wakifanya kazi kwa moyo, kujitolea na kukesha kuhakikisha shughuli mbalimbali za Serikali zinatekelezwa kwa wakati na kwa mafanikio makubwa.
Naye Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo anayesimamia Fedha za Umma, Bi. Amina Khamis Shaaban alisisitiza Wizara hiyo kuendelea kusimamia ukusanyaji wa fedha za ndani ili kuwezesha nchi kutekeleza miradi mbalimbali ya maendeleo.
Aidha alihimiza watumishi wa Wizara hiyo kusimamia upatikanaji wa mikopo nafuu ili kuiwezesha nchi kutumia fedha hizo kama kichocheo cha kujenga uwezo wa ndani na kujinasua kwenye utegemezi wa muda mrefu.
Bi. Amina aliongeza kuwa katika kupunguza utegemezi huo suala la Ubia kati ya Sekta ya Umma na Binafsi (PPP) ni muhimu, na kusisitiza watumishi wa Wizara hiyo hususan wale wanaohusika na PPP kuibua na kusimamia kikamilifu miradi ya ubia.
Kwa upande wao Mhasibu Mkuu wa Serikali CPA (T), Leonard Mkude na Mkaguzi Mkuu wa Ndani, Bw. Benjamin Magai, walisema kuwa ushirikiano uliotolewa na watumishi umewezesha wizara kukamilisha majukumu ya kimalipo katika mwaka wa fedha 2024/25.
Aidha, waliongeza kuwa miradi mbalimbali ya maendeleo imeweza kutekelezwa pamoja na kukamilisha ufuatiliaji na tathmini katika miradi hiyo.
Katika kikao hicho viongozi walihimiza utulivu, uwajibikaji, uadilifu, kutunza siri na mali za umma pamoja na kujilinda katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu wa Serikali huku wakisisitiza watumishi hao kushiriki zoezi hilo kikamilifu kwa maslahi mapana ya nchi.