Na Ashrack Miraji Fullshangwe Media
Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa, Ismail Ally Usi, ametoa salamu za rambirambi kwa wananchi wa Wilaya ya Same na Mkoa wa Kilimanjaro kufuatia ajali mbaya ya barabarani iliyosababisha vifo vya watu kadhaa, akisema ni msiba mkubwa kwa taifa zima.
Akizungumza wakati wa shughuli za mwenge wa Uhuru zilizofanyika wilayani Same, Ally alieleza masikitiko yake kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, akisema kwamba taifa zima linaungana nao katika kipindi hiki kigumu cha maombolezo.
“Ni pigo kubwa kwa wananchi wote, ndugu, jamaa na marafiki kupoteza maisha ya wapendwa wao katika ajali hii. Kama kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru, ninatoa pole kwa niaba ya Serikali na kwa niaba ya mbio hizi za kitaifa,” alisema Ally.
Aidha, alitoa wito kwa jamii kuendelea kuwa na moyo wa uvumilivu na kuendelea kuwaombea marehemu wote wapumzike kwa amani, huku akisisitiza kuwa mshikamano wa kitaifa ni nguzo muhimu wakati wa majonzi kama haya.
Ajali hiyo, ambayo ilitokea hivi karibuni katika maeneo ya Wilaya ya Same, ilihusisha gari la abiria na kusababisha majeruhi na vifo, hali iliyoleta huzuni kubwa kwa familia husika na taifa kwa ujumla.
Mwisho wa hotuba yake, Ally alihimiza madereva kuwa waangalifu barabarani na kuzingatia sheria za usalama wa barabarani ili kuepuka matukio kama hayo yajayo ambayo huacha athari kubwa kwa jamii.