-Mitungi ya gesi 330 kugaiwa bure kwa Watumishi Magereza Simiyu
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan amepongezwa kwa kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia kwa vitendo.
Pongezi hizo zimetolewa leo Julai 1, 2025 na Mjumbe wa Bodi ya Nishati Vijijini (REB), Lucas Malunde wakati akimwakilishi Mwenyekiti wa Bodi hiyo, Mhe. Balozi Meja Jenerali (mstaafu), Jacob Kingu katika hafla ya kugawa mitungi ya gesi ya kilogramu 15 pamoja na jiko la gesi la sahani mbili kwa Watumishi wa Magereza Mkoa wa Simiyu.
“Mei 8, 2024, Mhe. Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan alizindua Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia. Toka kuzinduliwa kwa mkakati huo, Serikali imefanya juhudi mbalimbali kuhakikisha Watanzania wanatumia nishati safi ya kupikia ili kuokoa mazingira pamoja na vifo vilivyokuwa vinatokana na matumizi ya nishati isiyokuwa safi na salama ya kupikia.
Mhe. Rais ameweza kutoa fedha zilizowezesha magereza zote nchini kuachana na matumizi ya kuni na kuanza kutumia nishati safi ya kupikia. Na leo tuko hapa kugawa mitungi ya gesi pamoja na majiko yake kwa Watumishi wa Magereza. Zote hizi zikiwa ni juhudi za Mhe. Rais kuhakikisha Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia unatekelezwa kwa vitendo,” amesema Mjumbe huyo wa Bodi.
Awali akitoa taarifa kuhusu mradi huo, Kaimu Meneja Usaidizi wa Kiufundi kwa Wawekezaji Miradi kutoka Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Emmanuel Yesaya amesema kuwa jumla ya mitungi ya gesi ya Kilogramu 15 na majiko ya gesi ya sahani mbili 330 itagaiwa kwa Watumishi wa Magereza Mkoa wa Simiyu.
Kwa upande wake Mkuu wa Magereza Mkoa wa Simiyu, SACP Lugano Msomba ameishukuru Serikali kupitia REA kwa kuwawezesha Watumishi wa Magereza kupata nishati safi ya kupikia na kuahidi kuwa watakuwa mabalozi kwa wengine katika kampeni hiyo.