Na Silivia Amandius – Bukoba
Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Bukoba, Ndugu Julius Shulla, amezindua rasmi zoezi la ugawaji wa chanjo ya kuku kwa wataalamu wa mifugo ngazi ya kata, katika hafla iliyofanyika tarehe 1 Julai 2025, katika makao makuu ya halmashauri hiyo.
Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Ndugu Shulla alieleza kuwa chanjo hiyo imetolewa bure na Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi, kwa lengo la kuwalinda wafugaji dhidi ya hasara zinazotokana na magonjwa ya kuku. Alimshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuwekeza katika sekta ya mifugo na kuwajali wafugaji wadogo.
“Tunamshukuru sana Mhe. Rais kwa kutupatia chanjo hii bure. Hii ni fursa kubwa kwa wafugaji wote, hivyo nawasihi maafisa mifugo kuitumia ipasavyo kwa kuwafikia wafugaji wote waliopo kwenye maeneo yao,” alisema Shulla.
Amesisitiza kuwa zoezi la chanjo litafanyika kuanzia Julai 1 hadi Julai 15, 2025, na kila afisa mifugo anatakiwa kutekeleza jukumu hilo kwa uaminifu na weledi mkubwa kama ambavyo wamekuwa wakifanya awali.
Chanjo hiyo aina ya Tatu Moja imelenga kukinga kuku na bata dhidi ya magonjwa hatari ikiwemo Mdondo (Newcastle), Ndui (Fowl Pox), na Mafua ya kuku (Infectious Coryza), ambayo yamekuwa yakisababisha vifo vya ndege na hasara kwa wafugaji nchini.
Zoezi hili ni sehemu ya kampeni ya kitaifa inayotekelezwa katika halmashauri zote nchini, na linatarajiwa kuleta matokeo chanya katika kuinua afya ya mifugo na kipato cha wafugaji. Wananchi na wafugaji wametakiwa kujitokeza kwa wingi kufanikisha zoezi hilo.