Na Mwandishi Wetu
CHUO cha Ufundi Stadi VETA Kipawa jijini Dar es Salaam, kimeanzisha rasmi fani mpya ya mafunzo ya kufunga chupa za vinywaji kwa kutumia tekolojia ya kisasa, ikiwa ni sehemu ya juhudi za serikali na Mamlaka hiyo kuwawezesha vijana wa Kitanzania kuajirika katika sekta ya viwanda na kuboresha maisha yao kiuchumi.
Akizungumza katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba yanayoendelea katika viwanja vya Julius Nyerere, Mwalimu wa wa Chuo cha VETA Kipawa, Joshua Mwamkusi amesema fani hiyo mpya ni rafiki kwa vijana na inalenga kuwaandaa kwa soko la ajira linalohitaji ujuzi wa vitendo.
Amesema fani hiyo inamuwezesha kijana kupata maarifa ya kufunga chupa za vinywaji kwa ustadi na kwa viwango vya kimataifa, jambo ambalo linamfungulia mlango wa kuajiriwa katika viwanda vilivyopo nchini na hata kujiajiri mwenyewe,” amesema Bw. Mwamkusi.
Ameongeza kuwa mafunzo hayo yanayotolewa kwa muda mfupi yanalenga kutoa ujuzi wa moja kwa moja unaoweza kutumika mara moja kwenye mazingira ya kazi. Hivyo, vijana wanaohitimu wanakuwa tayari kuingia kwenye ajira au kuanzisha miradi yao wenyewe na kuendelea na uzalishaji
Mwamkusi amesema sifa za msingi kwa waombaji wa kozi hiyo ni kuwa wamehitimu angalau kidato cha nne, na wawe wamepata mafunzo ya awali au wana uzoefu katika fani ya Teknolojia ya Habari (IT), Umeme au Ufundi Mitambo (Mechanics).
Ametoa wito kwa wazazi, walezi na vijana nchini kuchangamkia fursa hiyo adhimu inayotolewa na VETA Kipawa kwa kuwa ni njia ya moja kwa moja ya kuelekea mafanikio ya kiuchumi, hasa katika kipindi hiki ambacho Tanzania inaelekea kwenye uchumi wa viwanda.
“Wazazi wanapaswa kuwahamasisha watoto wao kujiunga na mafunzo haya. Elimu ya ufundi imeendelea kuthibitika kuwa njia madhubuti ya kupunguza tatizo la ajira na kuwawezesha vijana kujitegemea,” amesisitiza.
Maonesho ya Sabasaba hutoa fursa kwa taasisi kama VETA kuonyesha huduma na mafunzo mbalimbali wanayotoa, huku wakitoa elimu kwa wananchi kuhusu nafasi zilizopo za mafunzo ya ufundi stadi. Fani hii mpya ya kufunga chupa ni miongoni mwa ubunifu wa hivi karibuni unaolenga kushirikiana na viwanda vya ndani katika kuongeza ajira na uzalishaji nchini.