EMMANUEL MBATILO, MICHUZI TV
SHIRIKA la Viwango Tanzania (TBS) limepokea tuzo kutoka Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope, kutokana na desturi waliyojiwekea kutoa mchango wao kwa watu mbalimbali hususani jamii ya watu wenye ulemavu.
Akizungumza leo Julai 03,2025 Jijini Dar es salaam, Mkurugenzi Mkuu TBS Dkt.Ashura A Katunzi amesema shirika hilo licha ya kushughulika na viwango pamoja na ukaguzi wa bidhaa mbalimbali sokoni lakini pia linatimiza wajibu wake katika kugusa jamii kwa kutekeleza sera ya kurudisha kwa jamii (CSR Policy) kwa jamii mbalimbali ikiwemo watu wenyeulemavu.
Aidha Dkt. Katunzi ametoa shukurani zake kwa tuzo hiyo kwani imeonesha kutambuliwa kwa mchango wa TBS kwenye jamii ya watu wenye ulemavu kupitia jitihada walizozifanya kwa kipindi cha zaidi ya miaka 15.
Dkt.Katunzi amesema TBS imekuwa ikitoa misaada kwa jamii katika nyanja mbalimbali ikiwemo elimu pamoja na afya ya usaidizi kwa watu wenye ulemavu katika vipindi tofauti tofauti.
“Katika kipindi cha mwaka 2024/2025 TBS imewezesha makundi mawili ya watu wenye ulemavu katika vifaa,makundi mawili ya Afya katika ujenzi wa kituo cha afya pamoja na makundi manne ya shule katika ujenzi wa madarasa”Amesema.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi ya Foundation for Disabilities Hope Maiko Salali ameishukuru na kuipongeza TBS kwa kazi inayoifanya kwa kuweka ujumuishaji wa makundi yote ikiwemo walemavu katika utoaji wa huduma.
Salali ameeleza kuwa TBS imekuwa taasisi ya mfano wa kuigwa kwa juhudi zake kwa watu wenye ulemavu kwa kujenga mfumo jumuishi ambao haliachi kundi hilo nyuma,ambapo amezisihi taasisi nyingine kuiga mfano huo.
TBS kwa kujali maslahi ya Jamii imeweka kipaumbele suala la kurudisha kwa jamii ambapo imeahidi kuendelea kufanya suala hilo la kutoa msaada kuwa la msingi.