Tunduru-Ruvuma.
Baadhi ya wakulima wa zao la korosho katika Tarafa ya Nakapanya Wilaya ya Tunduru Mkoani Ruvuma,wamepongeza mpango wa Serikali wa kutoa bure viuatilifu vilivyowezesha kuongeza uzalishaji wa zao hilo mashambani na kujikwamua na umaskini.
Wakulima hao wamesema,viuatilifu hivyo vimesaidia sana kuzalisha korosho zilizobora na kukufua ndoto za wakulima ambao awali walikata tamaa kutokana na kushindwa kumudu gharama kubwa ya viuatilifu na pembejeo zilizokuwa zinauzwa kwa bei ya juu.
Mwenyekiti wa Chama cha msingi cha ushirika Mtetesi Amcos Adam Rashid,ameipongeza Serikali ya awamu ya sita kwa kuwathamini na kuwekeza nguvu kubwa kwa wakulima wadogo kwa kuwapa viuatilifu ambavyo vimerahisisha shughuli zao za kilimo.
Alisema,kabla ya kuanza kutoa pembejeo za ruzuku kwenye zao la korosho uzalishaji ulikuwa mdogo kwa sababu baadhi yao walishindwa kumudu gharama ya pembejeo kutokana na kuwa na kipato kidogo.
Adam,ameishukuru Serikali kupitia Wizara ya kilimo kusimamia soko la mazao ya kimkakati yanayouzwa kupitia mfumo wa soko la bidhaa(TMX)ambao umesaidia kupata soko la uhakika na bei nzuri ya mazao wanayozalisha.
“awali wakulima hatukufaidika na jasho la kazi zetu kwani kulikuwa na utofauti mkubwa wa bei kati ya chama kimoja na kingine wakati mazao ni yale yale,jambo hili lililotukatisha tamaa sana sisi wakulima”alisema Adam.
Mkulima mwingine anayehudimiwa na Chama cha msingi cha Ushirika Namitili kilichopo katika kijiji cha Nakapanya Issa Makokola alisema,katika kipindi cha miaka minne uzalishaji wa zao la korosho umeongezeka mara dufu kutokana na wakulima kupata pembejeo ikiwemo zinazotolewa bure na Serikali kupitia Bodi ya Korosho Tanzania.
Ameomba mpango huo uendelee kwa kuwa manufaa yake ni makubwa na umehamasisha wananchi walioanza kukata tamaa ya kuendelea na kilimo cha zao la korosho kufufua na kuongeza ukubwa wa mashamba yao.
“kabla serikali ya awamu ya sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan kuingia madarakani,uzalishaji ulikuwa chini ya tani 300 lakini sasa uzalishaji umeongezeka hadi kufikia wastani wa tani 1,580 hadi 2,000 kwa mwaka “alisema Makokola.
Esta Lwemba alisema,utaratibu wa malipo ya fedha kwa wakulima baada ya kuuza korosho na mazao mengine ya kimkakati umekuwa mzuri,kwani wanalipwa kati ya siku tatu hadi tano tofauti na miaka ya nyuma ambapo utaratibu wa malipo haukuwa rafiki.
Meneja wa Namitili Amcos Issa Wajika,ameipongeza idara ya Ushirika Halmashauri ya Wilaya Tunduru na Chama kikuu cha Ushirika(Tamcu Ltd)kusimamia vizuri ugawaji wa viuatilifu kwa wakulima na kusimamia minada ya korosho,ufuta na mbaazi inayofanyika katika maeneo mbalimbali.
Alisema,iwapo Serikali itaendelea na utaratibu huo,wakulima wengi zaidi wataendelea kujikita kwenye kilimo hivyo kuongezeka kwa uzalishaji wa zao hilo katika Mkoa wa Ruvuma.
Alisema,katika msimu wa kilimo 2021/2022 walipokea salfa mifuko 5,000 msimu 2022/2023 mifuko 6,000 msimu wa kilimo 2023/2024 mifuko 9,800 na msimu wa mwaka 2025/2026 tayari wamepokea salfa jumla ya mifuko 15,528 iliyogawiwa kwa wakulima.