AWASHAURI VIJANA KUJIANDAA NA UZEE
Na WMJJWM – Mwanza
Katibu Mkuu wa Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. John Jingu ameitaka jamii kushiriki kikamilifu katika kuwatunza wazee wao, kuwaheshima, kuwaangalia na kulinda dhidi ya vitendo vya kikatili.
Dkt. Jingu ameyasema hayo Julai 03, 2025 alipotembelea Makazi ya Wazee cha Bukumbi yaliyopo mkoani Mwanza kwa lengo la kuwajulia hali wazee wanaoishi katika Makazi hayo pamoja na kusikiliza changamoto zinazowakabili.
Dkt. Jingu ametoa wito mahsusi kwa vijana na jamii kwa ujumla kujiandaa kwa maisha ya uzee kwa kutumia vizuri rasilimali walizonazo wakiwa bado vijana.
“Ni muhimu vijana wawe na mtazamo wa muda mrefu kwa kuwekeza katika familia, mahusiano mema na miradi ya kiuchumi ambayo itawasaidia wanapoingia uzeeni. Ujana ni hatua ya maandalizi ya uzee, tusikimbie wajibu huu.” amesisitiza Dkt. Jingu.
Katika ziara hiyo, Dkt. Jingu amehimiza pia wazee kushiriki katika Uchaguzi Mkuu pamoja na fursa mbalimbali za kiuchumi, ikiwemo zile zinazotolewa kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Ununuzi wa Umma (PPRA).
Katika hatua nyingine, Dkt. Jingu ametembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mahabusu ya watoto jijini Mwanza ambapo ameeleza kuridhishwa na hatua iliyofikiwa kwani mradi huo umefikia asilimia 90 ya utekelezaji. Ujenzi wa mahabusu hiyo ni sehemu ya utekelezaji wa mapendekezo ya Tume Maalum iliyoundwa ili kuboresha Taasisi za haki jinai nchini hususan zinazohusiana na watoto.