Na Hellen Mtereko,Mwanza
Watu watatu wa jinsia ya kiume wakamatwa na Jeshi la Polisi wakiwa wanaiba kwenye karakana ya vifaa vya umeme mali ya shirika la umeme Tanzania (TANESCO) iliyopo mtaa wa Isengeng’he Kata ya Mhandu Wilaya ya Nyamagana.
Watu hao walikuwa na gari yenye namba za usajili T.285 DWA aina ya Toyota Wishi rangi nyeusi waliingia katika karakana hiyo nakuanza kuiba vipuli vya umeme aina ya Polymeric na reflector jaketi tatu kisha kuvipakia ndani ya gari hilo.
Hayo yamebainishwa na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza Willibroad Mutafungwa wakati akitoa taarifa kwa waandishi wa habari.
Alisema wakati watuhumiwa hao wakiendelea kupakia vifaa hivyo ndani ya gari ndipo walinzi waliokuwa wanalinda eneo hilo walibaini uhalifu huo na kufyatua risasi hewani wakitumia silaha aina ya shot gun iliyosababisha wahalifu hao kutawanyika.
“Baada ya risasi kusika hewani askari wa jeshi la polisi waliokuwa doria walifika eneo hilo mara moja ndipo walipata taarifa ya tukio la wizi kutoka kwa walinzi wa neo hilo na baada ya kujiridhisha na taarifa hiyo walishirikiana kuwatafuta wahalifu na kufanikiwa kuwakamata wakiwa ndani ya eneo”, Alisema Kamanda Mutafungwa
Alieleza kuwa watuhumiwa waliokamatwa ni Venister Mladi (24) mkulima na mkazi wa mtaa wa Nyegezi Wilaya ya Nyamagana,Yusuphu Bilamata (25) fundi aluminium na mkazi wa mtaa wa usagara Wilaya ya Misungwi na Lugaila Ibrahimu (24) dereva tax mkazi wa kishiri ambae ndiye aliyekuwa anaendesha gari hilo.
Mtuhumiwa mmoja alikuwa na jeraha kichwani sehemu za utosini ambalo alilipata baada ya kuangukia vyuma vilivyokuwa kwenye karakana hiyo wakati anakimbia asikamatwe.
“Watuhumiwa wawili walipelekwa kituo cha polisi nyakato kwa hatua zaidi za kisheria na majeruhi alipelekwa hospitali ya Sekoutoure kwa matibabu na ilipofika majira ya saa kumi na moja asubuhi alifariki dunia”,

