Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mhe. Hamza S. Johari amemkabidhi Juzuu za Sheria zilizofanyiwa Urekebu toleo la Mwaka 2023 Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Jaji George M. Masaju Ofisini kwake Jijini Dodoma tarehe 03 Julai, 2025.
Akizungumza wakati wa kukabidhi Juzuu hizo, Mwanasheria Mkuu wa Serikali amemshukuru Jaji Mkuu kwa mchango ambao Mahakama umeutoa katika kufanikisha zoezi la Urekebu wa Sheria ambapo ameeleza kuanza kutumika kwa sheria kutairahisishia Mahakama wakati wa kutekeleza majukumu yake ya utendaji haki kwa wananchi.
*“Mhe. Jaji Mkuu baada ya kukamilika kwa zoezi la urekebu na Mhe. Rais alizindua na alitoa tamko kwamba Sheria hizi zianze kutumika kuanzia tarehe 1 Julai, hivyo tumekuja na timu yangu kuja kukukabidhi rasmi Juzuu hizi zilizofanyiwa Urekebu.”* Amesema Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Aidha, Mwanasheria Mkuu wa Serikali ameeleza kuwa mradi wa urekebu wa sheria umefanyika kwa kutumia rasilimali za fedha za ndani na rasilimali watu wa ndani, tofauti na ilivyokuwa miaka ya nyuma ambapo mradi huo ulikuwa ukiendeshwa na Wahisani.
*“Kitu kizuri ni kwamba huu mradi tumeufanya kwa fedha zetu za ndani na hata publisher ni wa ndani, kuanzia sasa hatutasubiri tena miaka kumi zile annual supplement sasa tutahakikisha tunazitoa ipasavyo ili ikifika miaka 10 mradi usiwe mkubwa sana”*. Ameeleza Mwanasheria Mkuu wa Serikali
Akipokea Juzuu hizo, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Jaji George M. Masaju ameishukuru Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kutambua mchango wa Mahakama katika kufanikisha zoezi hilo, ambapo ameeleza kuwa Mahakama ni mtumiaji mkubwa wa sheria hizo na zitasaidia katika utendaji kazi wa Mahakama.
*“Sisi kama Mahakama ni moja ya watumiaji wakuu kwasababu mambo mengi yanaishia mahakamani hivyo tukiwa na hizi Juzuu zitatusaidia sana.”* Amesema Jaji Mkuu wa Tanzania
Katika hatua nyingine Jaji Mkuu wa Tanzania ameipongeza Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali kwa kuukamilisha mradi wa urekebu wa sheria kwa kutumia rasimali fedha za ndani pamoja na kuzifanya sheria hizo kupatikana bure kwa njia ya mtandao na kuwasaidia watumiaji wengi kuzipata kwa urahisi.
Awali, Mwandishi Mkuu wa Sheria, Bw. Onorius Njole amempongeza Jaji Mkuu wa Tanzania kwa mchango wake katika kukamilisha zoezi hilo tangu akiwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, ambapo amesema wamekabidhi seti ya Juzuu za sheria za nchi 20 ambayo ina jumla ya sheria kuu 446.
Vilevile Mwandishi Mkuu wa Sheria amesema Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali imetekeleza maagizo ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan ya kuhakikisha Sheria hizi zinapatikana, ambapo sheria hizo zinapatikana katika mfumo wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali ujulikanao kama OAG-MIS.
*“Kama alivyoelekeza Mhe. Rais wakati wa uzinduzi kuwa sheria hizi ziwe accessible pamoja kwa kupatikana kwa njia ya kuuzwa na mchapishaji Mkuki na Nyota na pia sheria hizi zinapatikana katika mfumo wa OAG-MIS wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali”.* Amesema Mwandishi Mkuu wa Sheria
Juzuu za Sheria zilizofanyiwa Urekebu toleo la mwaka 2023 zilisainiwa na kutolewa tamko na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan tarehe 23 Aprili, 2025 na zimeanza kutumika kuanzia tarehe 1 Julai, 2025.