Na Mwandishi Wetu
MFUKO wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umesikia hoja za wananchi kuhusu gharama za vifurushi vya bima za afya ambapo gharama hizo zimepungua
Hivi saa mtu anaweza kupata kifurushi cha Sh168,000 kwa mwaka sambamba na uwepo wa vifurushi mbalimbali ikiwemo vya watoto.
Hili linasemwa wakati ambao tayari utekelezaji wa sheria ya bima ya afya kwa wote umeanza huku utaratibu maalumu ukiwa umewekwa ili kuwafikia wale wasiokuwa na uwezo wa kumudu gharama ikiwemo kaya maskini.
Hayo ameyasema Meneja wa NHIF Ofisi ya Temeke, Cannon Luvinga wakati akizungumza na waandishi katika maonyesho ya 49 ya biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (DITF).
Amesema kupungua kwa bei hiyo kunalenga kuwafanya watu wengi zaidi kumudu gharama za matibabu ili kufanikisha utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.
“Mwazo watu waliona bei za vifurushi si rafiki, lakini tulikaa chini tumeweka bei rafiki na sasa watanzania wanachangamka katika kukiunga ili wawe na uhakika wa matibabu kwani tumesajili vituo zaidi ya 19,000 hivyo mtanzania aliyrjiunga na NHIF hatembei umbali mrefu kufuata huduma,” amesema.
Amesema kwenye Sh168,000 mtu anaweza kupata huduma kwa mwaka mzima huku akisema fedha hiyo ni ndogo na mtu anaweza kulipa kila mwezi.
“Bei zipo mbalimbali kulingana na ukubwa wa familia, umri na tunampa nafasi mtanzania kuunganisha familia yake, bei ya kifurushi inategemeana na ukubwa wa familia uliyonayo,” amesema.
Akizungumzia uwepo wao katika maonyesho hayo amesema mbali na kusikiliza changamoto mbalimbali za wateja pia watakuwa wakisajili wanachama wapya ambao wanatakiwa kuja na namba za Kitambulisho cha Taifa pekee ili waunganishwe.
“Kwa upande wa watoto mzazi anapswa kuja na cheti chake cha kuzaliwa ili aweze kuunganishwa. Pia upo utaratibu wa watu wanaotoka kaya maskini kuoata huduma hii kupitia Tasaf (Mfuko wa Maendeleo ya Jamii) amesema.
Amesema hili linaenda sambamba na kuweka utaratibu maalumu kwa ajili ya kaya maskini ili kuwaingiza katika mfumo wa bima.
“Lakini pia kuna kifurushi cha bima kwa wote kwa kaya masikini, chenye huduma 277, ambacho kitaanza kutumika kwa gharama ya Sh150,000 kwa kaya ya watu sita, sawa na Sh25,000 kwa kila mtu kwa mwaka. Hii ni gharama nafuu ukilinganisha na gharama halisi ya bima,”
Kutokana na kushushwa kwa bei za vifurushi, Serikali katika mwaka 2025/2026 ilipendekeza kuanzisha vyanzo vya mapato vinane kwa ajili ya kudhibiti maambukizi ya Virusi vya Ukimwi (VVU) na kugharimia bima ya afya kwa wote.
Hatua hiyo inatarajiwa kuongeza mapato ya Serikali kwa Sh586.4 bilioni.