Msafara wa baiskeli wa Twende Butiama Cycling Tour 2025 umeanza rasmi Julai 3, 2025, ukiwa na waendesha baiskeli zaidi ya 180 wakiwa njiani kuelekea Butiama. Safari hii ya kihistoria, yenye urefu wa zaidi ya kilomita 1,500 na inayotarajiwa kuchukua takribani siku 11, inalenga kumuenzi Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu JK Nyerere, kwa kuendeleza mapambano dhidi ya maadui watatu ambao ni Ujinga, Umasikini na Maradhi hapa nchini.
Ukidhmainiwa na Vodacom Tanzania PLC kwa kushirikiana na Benki ya Stanbic Tanzania, msafara huu umeanzia jijini Dar es Salaam na kwa siku 11 unategemewa kupita katika mikoa 11, ukibeba ujumbe wa matumaini na mabadiliko chanya.
Njiani, msafara huu unatoa huduma mbalimbali zenye kugusa maisha ya wananchi moja kwa moja. Hizi ni pamoja na kampeni kubwa za upandaji miti zinazolenga kupanda miti 50,000 ili kulinda mazingira, na kutoa msaada muhimu wa elimu kwa shule mbalimbali.
Msaada huu wa elimu unajumuisha ugawaji wa madawati 1,500 kwa shule 10 za msingi pamoja na baiskeli 50 kwa wanafunzi wanaoishi mbali na shule (hasa wasichana), ili kuwawezesha kufika shuleni kwa urahisi. Waendesha baiskeli wa kimataifa kutoka nchi mbalimbali za Afrika na hata Marekani na Ulaya wamejiunga na msafara huu, wakionesha ushirikiano wa kimataifa katika kuleta maendeleo.
Msafara wa huu unatarajiwa kufika Butiama tarehe 13 Julai, 2025, ukiacha kumbukumbu ya kudumu katika jamii nyingi zilizofikiwa. Lengo kuu la waandaaji ni kuwafikia Watanzania zaidi ya 700,000, wakiwemo watoto, vijana na wazee, na kuendeleza urithi wa Mwalimu Nyerere wa kupambana na ujinga, maradhi na umasikini.
Kampeni hii inaendelea kudhihirisha nguvu ya ushirikiano kati ya sekta binafsi na jamii katika kuleta mabadiliko chanya na endelevu kwa mustakabali bora wa Tanzania.