Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Pembejeo Bi. Mwanahiba Mzee, akitoa elimu kwa mwananchi aliyetembelea Banda la Taasisi hiyo, kufahamu fursa zitolewazo na Taasisi hiyo.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Pembejeo Bi. Mwanahiba Mzee, akizungumza katika mahojiano maalum na waandishi wa habari, kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba, yanayofanyika katika viwanja vya Julius Nyerere, Jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mfuko wa Pembejeo Bi. Mwanahiba Mzee, ametoa rai kwa wakulima kote nchini, kutumia fursa ya mikopo inayotolewa na mfuko huo, ili waweze kupata fedha kwa masharti nafuu na riba ndogo, zitakazowawezesha kuendeleza shughuli zao za kilimo.
Mkurugenzi huyo ametoa kauli hiyo katika mahojiano na waandishi wa habari, yaliyofanyika Julai 4, 2025, kwenye Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara Sabasaba, yanayoendelea katika viwanja vya Mwalimu Julius Nyerere Jijini Dar es Salaam.
Amesema kuwa fursa hiyo inawaangalia zaidi wakulima wadogo na wa kati, wenye ekari zisizozidi 50, na wale anaowanufaisha wakulima wenzie.
“Sisi tunawaangalia wale wakulima wadogo wenye ekari zisizozidi 50, lakini pia tunaangalia kama anawanufaisha wakulima wenzie” amesema.
Akizungumzia ushiriki wao kwenye Maonesho ya Sabasaba mwaka huu, Bi. Mwanahiba amesema wamejikita katika kutoa elimu ya mikopo wanayoitoa ambayo ni maalumu kwa wakulima wadogo, wachakataji mazao wadogo, na wale wote wanaofanya biashara katika mnyororo wa kilimo.
“Mikopo ya masharti nafuu na riba nafuu ni mikopo ambayo ni rafiki kwa wanachi wa kawaida.
“Maeneo ambayo tunatoa fedha za mikopo ni kuanzia shambani kwa maana kuanzia mtu anapoandaa shamba lake, pembejeo zote za kilimo, miundombinu ya umwagiliaji mpaka wakati anavuna, lakini pia tunatoa zana za kilimo kama power tiller”
Aidha, ameongeza kuwa, kwenye uchakataji wa mazao, wanatoa mashine mbalimbali ikiwa ni pamoja na zile zinazotumika kuchakata mafuta, mchele, uzalishaji wa unga na mvinyo, nakwamba Mfuko huo unawalenga hasa wakulima ambao wakienda kwenye taasisi za fedha wanakosa vigezo vya kupata mikopo kutokana na wengi wao kukosa hati itakayomuwezesha kupata mikopo hiyo.
Ameongeza kuwa, aina ya mikopo nafuu inayotolewa na Mfuko huo inawalenga vijana na wanawake, kutokana na kutokuwa na uwezo wa kupata mitaji na uzoefu, kwani wengi wao hawamiliki dhamana za kupata mikopo hiyo.
“Kwa wanawake na vijana tuna aina mkopo unaoitwa Mkulima Nafuu, ambayo tunakopesha kwa asilimia 4.5 kwa mwaka kwa vijana kuanzia miaka 18 hadi 40 kwa wanaume, na wanawake hadi umri wa miaka 65, na dhamana sio kipaumbele” ameongeza.
Mfuko wa Pembejeo unatimiza miaka 30 mwaka huu tangu kuanzishwa kwake, ambapo katika kipindi chote umekuwa kimbilio kwa wananchi mbalimbali na kuweza kukopesha jumla ya Shilingi Bilioni 95 kwa wakulima wadogo, pamoja na pembejeo yakiwemo matrekta zaidi ya 1,500, na kuhakikisha uwepo wa usalama wa chakula nchini, pamoja na kuongeza ajira kwa vijana wengi nchini nzima.
Afisa Uendeshaji Mkuu wa Mfuko wa Pembejeo, Mhandisi, Manolana Aloyce, (wa pili kulia), akisisitiza jambo, alipokuwa akizungumza na mwananchi aliyetembelea katika Banda la Mfuko huo, Maonesho ya 49 ya Sabasaba, Jijini Dar es laam.
Afisa Uendeshaji, Mfuko wa pembejeo Bw. Ally Wajihi, (wa kwanza kulia), akizungumza na baadhi ya wananchi waliotembelea katika banda hilo, kwenye naonesho ya Sabasaba, Dar es Salaam.