TOLEO la Sheria ambazo zimetafsiriwa kwa lugha ya Kiswahili zinatarajiwa kuanza kutoka ifikapo Agosti mwaka huu ikiwa baada ya hivi karibuni Rais Samia Suluhu Hassan kuagiza kutafsiriwa kwa sheria ili iweze kueleweka kwa urahisi na watu wa makundi yote.
Ameyasema hayo leo Julai 6, 2025 Mwandishi Mkuu wa Sheria, Onorius Njole, katika Maonesho ya 49 ya Kimataifa ya Biashara ‘sabasaba’ yanayoendelea Jijini Dar es Salaam.
Aidha Njole amesema kuwa sambamba na kuendelea na mchakato wa kukamilisha zoezi hilo pia Ofisi hiyo imefanya mabadiliko makubwa ya kuhakikisha sheria zilizopo zinatekelezeka na kuwafikia wananchi.
“Mpaka sasa tumefanya mabadiliko makubwa ya kuhakikisha tunakuwa na sheria zinazowafikia wananchi kama Sheria na ukamilifu wake na lugha ambayo wananchi wanaifahamu” amesema Njole.
Amesema kuwa ofisi hiyo imefanywa urekebu wa sheria mbalimbali ili ziweze kuendana na mahitaji ya sasa ya nchi “ tumefanya urekebu wa Sheria hizi kwa kuzikisanya sheria zote za nchi pamoja na kuingiza marekebisho ambayo yamekuwa yakifanyika kila wakati” amesema
Pamoja na hayo, amesema kuwa Serikali ipo katika mchakato wa kutengeneza mfumo wa sheria wa kusimamia matumizi ya Akili Mnemba (IA) na kubainisha kuwa mchakato huo utakapokuwa tayari utaandaliwa sheria.