Arusha, Tanzania — Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imezindua rasmi Programu Maalum ya Samia Extended Scholarship kwa Sayansi ya Data, Akili unde na Sayansi Shirikishi, ikiwa ni hatua thabiti ya kujenga uchumi wa maarifa unaoongozwa na vijana wenye vipaji vikubwa.
Akizungumza katika uzinduzi uliofanyika katika Chuo cha Nelson Mandela cha Sayansi na Teknolojia ya Afrika (NM-AIST), Prof. Kipanyula, Makamu wa Rais wa NM-AIST, alieleza fahari ya chuo hicho kushiriki moja kwa moja katika maandalizi ya kizazi kipya cha wataalamu wa teknolojia.
“Tunashukuru Wizara na Serikali kwa kuchagua NM-AIST kama kitovu cha maandalizi ya awali kwa wanafunzi hawa. Kwa kweli, tunajivunia kuwa sehemu ya historia ya kujenga taifa la wataalamu wa data science na AI,” alisema Prof. Kipanyula.
Naye Dkt. Amos Nungu, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (COSTECH), ambayo inaratibu utekelezaji wa programu hiyo, alisema kuwa huu si tu mpango wa masomo, bali ni tamko la kitaifa la kujenga taifa la maarifa.
“Tunachofanya leo si tu ufadhili wa masomo ni uwekezaji wa kizalendo. Kupitia Samia Scholarship, Tanzania inasema kwa sauti kuwa haitaachwa nyuma katika Mapinduzi ya Nne ya Viwanda,” alisema Dkt. Nungu.
Akitoa hotuba kuu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda, alisisitiza kuwa serikali imeanza kutekeleza kwa vitendo ahadi ya kukuza matumizi ya akili unde kama ilivyoainishwa kwenye bajeti ya mwaka huu.
“Kwa mara ya kwanza, haijalishi uwezo wa familia yako, bali uwezo wa kichwa chako,” alisema Prof. Mkenda.
“Ukiwa miongoni mwa walioteuliwa, usiombe chuo kingine mwaka huu. Njoo NM-AIST uandaliwe kwa miezi kumi. Utapewa laptop, kufundishwa kozi ya awali, na kuandaliwa kwa maisha ya kimataifa.”
Katika awamu ya kwanza, wanafunzi 700 bora kutoka matokeo ya mitihani ya taifa watachaguliwa. Kati yao, wanafunzi 50 waliofanya vizuri zaidi katika tahasusi ya sayansi na Hisabati ya Juu (Advanced Mathematics) watapelekwa vyuo bora vya kimataifa kama MIT (Marekani), Oxford (Uingereza), IIT Madras (India) na Peking University (China). Wanafunzi 650 watasoma hapa nchini kwa ufadhili kamili wa serikali.
Prof. Mkenda alisisitiza zaidi: “Hatuwezi kujifungia. Lazima tukafuate elimu mahali popote ilipo. Tunataka vijana wetu wakachote maarifa huko na walete nyumbani.”
Programu hii inatekelezwa kwa ushirikiano kati ya NM-AIST, COSTECH, Wizara ya Elimu, wataalamu wa diaspora na taasisi za kimataifa, ikiwa ni sehemu ya dhamira ya Rais Samia Suluhu Hassan ya kuiweka Tanzania katika ramani ya maarifa ya dunia.