Taasisi ya Elimu Tanzania (TET) yaendelea kutoa elimu kwa wadau waliojitokeza katika maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba kuhusu maboresho yaliyofanyika katika Mitaala.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi hiyo Dkt. Aneth Komba alipotembelea katika banda la TET leo Julai 9, 2025, huku akisisitiza lengo la maboresho ya Mtaala huo ni kupata mhitimu mwenye uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa.
Ameendelea kusema, TET imejipanga kuhakikisha Mtaala ulioboreshwa unatekelezwa kwa usahihi kwa asilimia zote, huku akitoa wito kwa wadau kuendelea kukaribia kwenye banda la TET kununua vitabu vya kiada vya Mtaala huo.
Sambamba na hilo Dkt. Komba amesema, Taasisi ya Elimu Tanzania inatekeleza Mitaala kupitia teknolojia mbalimbali ikiwemo maktaba mtandao inayomruhusu mtumiaji kujisomea vitabu mbalimbali ya Mtaala ulioboreshwa na machapisho mengine bila matumizi ya bando.
Pia, Dkt. Komba amesema, maboresho yaliyofanyika katika Mtaala ni pamoja na eneo la maadili na uzalendo linalofundishwa kwa lugha ya kiswahiki kuanzia katika ngazi zote, poa katika matumizi ya lugha na Teknolojia.
Aidha, Dkt. Komba amesema, TET inaendelea kusherekea miaka 50, hivyo ametoa wito kwa wananchi kuendelea kuchangia kampeni ya “Kitabu Kimoja, Mwanafunzi Mmoja, Mpe Kitabu gusa ndoto” ili kuhakikisha kila mtoto anakitabu chake na kompyuta yake.
Amewaomba kuchangia kupitia nambari 994040118259 yenye jina la Taasisi ya Elimu Tanzania
Kwa upande mwingine, Dkt. Komba amesema, katika kuendelea kufikisha elimu mbali zaidi kwa wananchi Taasisi ya elimu Tanzania imezindua Television (TET SOMA KWANZA TV) inayolenga kutoa elimu kuhusu mitaala na shughuli nyingine katika Sekta ya elimu kwa ujumla.
Katika ziara yake Sabasaba,Dkt.Komba alipata nafasi ya kutembelea mabanda ya Taasisi kadhaa zilizopo katika maonesho hayo.