Baadhi ya Wazazi wa Kata ya Hasanga Wilaya ya Mbozi Mkoani Songwe wametakiwa kuwalinda watoto wao kama wanavyozilinda simu zao baada ya watoto wanaotoka katika kata hiyo kupotea na kuletwa kituo cha Polisi Vwawa.
Rai hiyo ilitolewa Julai 09, 2025 na Mkuu wa Kituo cha Polisi Vwawa Mrakibu wa Polisi (SP) Veronica Myovela na kuwaambia kuwa katika dunia ya sasa inayotawaliwa na teknolojia, simu za mkononi zimechukua nafasi kubwa katika maisha yetu ya kila siku, tunazibeba kila mahali, tunazilinda dhidi ya kuharibika, kuibiwa au kupotea ikiwa ni pamoja na tuziweka nywila na hata kuzikatia bima kwa ajili ya usalama wake, lakini hatuwapi watoto wetu uangalizi kama huu jambo linalopelekea watoto kufanyiwa vitendo vya ukatili na kujiingiza katika uhalifu na kupoteza malengo ya masomo yao.
“Watoto ni msingi wa jamii yetu na urithi wa taifa la kesho ila kutokana na ukosefu wa malezi bora na uangalizi kwa sababu Wazazi na walezi wengi wamepindukia kutumia muda mwingi kwenye simu huku watoto wakiachwa bila uangalizi wa karibu au mawasiliano ya moja kwa moja mpaka kusababisha watoto kupotea na kufanyiwa vitendo vya ukatili kitendo ambacho sio sawa” alisema SP Myovela.
“Ni wajibu wa kila Mzazi/Mlezi na jamii kwa ujumla kuhakikisha mnawalinda na kuwalea watoto kwa upendo, umakini na ukaribu mkubwa hata zaidi ya jinsi mnavyolinda simu zetu” alisisitiza SP Myovela.
Vilevile SP Myovela, aliwataka Wazazi hao kuwasikiliza, kuwapa muda wa kuwa nao karibu na kuwaelekeze mambo mema ikiwa ni pamoja na kuwafuatilie katika maisha yao ya kila siku na sio kusubiri matatizo yajitokeze ndipo wachukue hatua, mnatakiwa kujiuliza kama mnakumbuka kuchaji simu kila usiku, kwa nini msikumbuke kuzungumza na watoto wenu inatakiwa msumbuke na watoto wenu kama simu zetu zinapopotea, pia mfuatilie mtoto anapoanza kubadilika tabia au anapokosa tabasamu ili kujua nini chanzo na kuweza kupata ufumbuzi wa tatizo linalomkabili kwa manufaa ya maisha yake ya baadae.