Tunduma, Songwe
Watendaji wa Kata kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Kibaha wameendelea na ziara yao ya kikazi katika Halmashauri ya Mji Tunduma kwa lengo la kujifunza mbinu mbalimbali za ukusanyaji wa mapato, hususan katika eneo la maegesho ya magari.
Katika ziara hiyo ya mafunzo, watendaji hao walipata elimu ya kina kuhusu mbinu bora za ukusanyaji wa mapato ya maegesho ya magari. Mafunzo hayo yamelenga kuwajengea uwezo wa kitaalamu na kimkakati ili kuongeza ufanisi wa ukusanyaji mapato katika Manispaa ya Kibaha.
Baada ya mafunzo ya darasani, wamepata fursa ya kutembelea maeneo mbalimbali ya maegesho ya magari yanayosimamiwa na Halmashauri ya Mji Tunduma, ambapo walijionea kwa vitendo namna halmashauri hiyo inavyoweza kukusanya mapato makubwa kutokana na chanzo hicho cha mapato.
Watendaji hao pia walitembelea eneo la mpaka wa Tanzania na Zambia na kushuhudia kwa vitendo jinsi mapato ya maegesho ya magari yanavyosaidia kuongeza pato la taifa kupitia shughuli za usafirishaji na biashara mpakani.
Vilevile, wamejionea mafanikio ya utekelezaji wa miradi ya maendeleo inayofadhiliwa na mapato hayo, ikiwemo ujenzi wa shule nne za sekondari za ghorofa ambazo zimejengwa kwa lengo la kupunguza changamoto ya wanafunzi kutembea umbali mrefu kufuata elimu ya sekondari.
Akizungumza mara baada ya mafunzo hayo mratibu wa mapato Manspaa ya Kibaha mwl Isihaka Mwalimu amesema amesema kuwa wamefurahishwa na mafunzo waliyoyapata na wamejipanga kuyatumia ipasavyo katika Manispaa ya Kibaha ili kuongeza mapato na kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi.
Ziara hiyo ni sehemu ya mkakati wa Manispaa ya Kibaha wa kuboresha ukusanyaji wa mapato ya ndani kwa lengo la kuongeza uwezo wa kifedha wa halmashauri na kuchochea maendeleo.