KIKAO cha Viongozi wa CCM wakiongozwa na Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,pamoja na Msafara wa Viongozi kutoka China chini ya kiongozi wao Makamu Mwenyekiti wa CPPCC na Mkuu wa Msafara Prof. Jiang Zuojun, wakizungumza katika Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.
NAIBU Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt.Mohamed Said Dimwa,akizungumza na Viongozi hao kutoka China katika kikao kilichofanyika Afisi Kuu ya CCM Zanzibar Kisiwandui.
Makamu Mwenyekiti wa CPPCC na Mkuu wa Msafara Prof. Jiang Zuojun,akizungumza masuala mbalimbali ya kuimarisha ushirikiano baina ya CPC na CCM pamoja na mikakati mingine ya kiutendaji.
Picha ya Pamoja baina ya Viongozi wa CCM Zanzibar na Msafari wa Ugeni kutoka China mbele ya OfisiKuu ya CCM Kisiwandui Zanzibar.
……..
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar.
Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dkt. Mohamed Said Dimwa, amesema Chama Cha Mapinduzi kinajivunia kuimarika kwa mahusiano ya kisiasa,kiuchumi na kijamii baina ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China.
Hayo aliyasema wakati akizungumza na msafara wa wageni kutoka nchini China waliofika Ofisini kwake Afisi Kuu ya CCM Kisiwandui kwa lengo la kujadili na kuzungumzia masuala mbalimbali ya kimaendeleo baina ya CCM na CPC.
Katika mazungumzo hayo kwa pande zote mbili zilijadiliana kwa undani namna ya kuendeleza uhusiano wa muda mrefu na wa kihistoria, uliojengwa juu ya misingi ya mshikamano wa vyama vya ukombozi, usawa na maendeleo ya pamoja.
Dkt. Dimwa alieleza kuwa uhusiano kati ya Tanzania na China ulianza kustawi baada ya Mapinduzi ya Zanzibar ya mwaka 1964, na kuimarika zaidi baada ya Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
Akisisitiza kuwa historia hiyo imejengwa juu ya misingi ya mshikamano wa kimapinduzi, alikumbusha namna China ilivyokuwa mshirika wa kweli wa Tanzania katika kipindi kigumu cha ukoloni, ukombozi na ujenzi wa taifa jipya.
Katika hotuba yake, Dkt. Dimwa alitaja ushirikiano wa kidiplomasia kati ya Tanzania na China kama mfano wa mafanikio ya sera ya kutoegemea upande wowote.
Alisisitiza kuwa China imekuwa mdau mkubwa katika kulinda uhuru na kujitegemea kwa Tanzania, sambamba na kuunga mkono sera zake za kijamaa.
Dkt. Dimwa alieleza kuwa ushirikiano kati ya China na Tanzania haujaishia katika diplomasia tu, bali umeenea katika maeneo mengine muhimu ya kipaumbele kama ulinzi na usalama, afya, elimu, miundombinu, utalii, kilimo, michezo na biashara.
Alitoa pongezi kwa juhudi za serikali ya China, kupitia chama cha CPC, katika kusaidia miradi ya maendeleo, hasa katika kujenga Hospitali, Barabara, na Vituo vya afya, sambamba na kutoa nafasi za masomo na mafunzo kwa vijana wa Kitanzania wa fani mbalimbali za kipaumbe.
Akizungumzia ushirikiano wa kisiasa, Dkt. Dimwa alieleza kuwa uhusiano wa kihistoria kati ya CPC na CCM unaendelezwa kwa mafunzo ya viongozi, kubadilishana uzoefu wa uongozi na kushauriana juu ya sera za maendeleo.
“Vyama hivI viwili vinashirikiana katika kusimamia ajenda za kisiasa zinazolenga ustawi wa wananchi na kuhimiza maadili ya uzalendo, mshikamano na maendeleo jumuishi”,alieleza Dkt.Dimwa.
Kuhusu hali ya kisiasa ya ndani, Dkt. Dimwa alieleza kuwa CCM inaendelea na mchakato wa uchaguzi wa ndani kwa ajili ya kupata wagombea wa nafasi za Ubunge, Uwakilishi na Udiwani watakaopeperusha bendera ya CCM katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Aliongeza kuwa chama hicho kimejipanga kwa ushindi mkubwa kutokana na utekelezaji mzuri wa Ilani ya mwaka 2020/2025, na kwamba wanatarajia kuendeleza mafanikio hayo kupitia Ilani mpya ya 2025/2030, itakayozingatia mahitaji ya wananchi wote bila kujali tofauti za kisiasa, kidini au kikabila.
Dkt. Dimwa alitumia fursa hiyo kuishukuru CPC na Rais Xi Jinping kwa kuendeleza ushirikiano huo, na kutoa wito kwa China kuendelea kutoa mafunzo ya kiutendaji, nafasi za masomo, na ujenzi wa uwezo kwa watumishi wa umma, sekta binafsi, pamoja na viongozi na watendaji wa CCM na jumuiya zake.
Kwa upande wake, Prof. Jiang Zuojun, ambaye ni Makamu Mwenyekiti wa CPPCC na mkuu wa msafara wa China, alieleza kuwa lengo la ziara yao ni kujadili kwa kina namna ya kuendeleza mipango ya pamoja ya maendeleo baina ya China na Tanzania, kwa kuzingatia masuala ya sayansi, teknolojia, ubunifu, uongozi, matumizi bora ya rasilimali za bahari, uwekezaji na utalii.
Alisisitiza kuwa China ina dhamira ya kuendelea kusaidia Tanzania katika sekta zenye kipaumbele kama kilimo cha kisasa, afya, elimu, miundombinu, na kuongeza fursa za masomo kwa vijana wa Kitanzania ili kuongeza wataalamu na maarifa katika nyanja muhimu za karne ya 21.