Na Sophia Kingimali.
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt.Damas Ndumbaro amipongeza ofisi ya mwandishi mkuu sheria kwa kuendelea kufasili sheria kutoka lugha ya kiingereza na kuziweka katika kiswahili ili kusaidia wananchi kuweza kuzielewa sheria za nchi.
Akizungumza mara baada ya kutembelea banda la ofisi hiyo lililopo katika maonesho ya 49 ya Kimataifa ya biashara leo julai 11,2025 amesema ofisi hiyo ni muhimu kwani bila ya ofisi hiyo hakuna sheria itakayokwenda bungeni kutungwa.
“Hii ni ofisi muhimu sana bila ofisi hii hakuna sheria inayokwenda bungeni kutungwa,hakuna sheria itakayofanyiwa marejebisho bungeni wala hakuna sheria ndogo itakayotungwa wala kufanyiwa urekebu”,amesema.
Aidha Dkt Ndumbaro ameongeza kuwa mpaka sasa wameweza kufasili sheria kutoka kiingereza kwenda Kiswahili jumla ya sheria 300 kati ya sheria 446.
Amesema katika mwaka huu wa fedha serikali imetenga bajeti ili waweze kufasili sheria zilizobaki 146 ili kukamilisha sheria zote 446 ili watanzania waweze kuzielewa kwani hiyo ndio kazi yao kuu.
“Hii ni ofisi muhimu sana kwani ikifa ofisi hii hata mahakama itavurugukiwa kwani itakuwa inatumia sheria ambazo hazipo sahihi,kazi ya ofisi hii muhimu katika mustakabali mzima wa kutunga na kuchakata sheria za nchi”.amehitimisha DK Ndumbaro.