Mwenyekiti wa Bodi katikati Bw. Leonard Mususa akizungumza na Wanahisa (hawapo pichani)
Mwanahisa akiuliza swali katika mkutano.
Baadhi ya wanahisa wakiwa katika mkutano.
……………
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa Kiwanda cha Bia cha Tanzania Breweries Public Limited Company (TBL Plc), Leonard Mususa leo ametoa taarifa ya maendeleo wanahisa waliowekeza kwenye kampuni hiyo.
Akitoa taarifa hiyo wanahisa nao walipata nafasi ya kuuliza maswali mbalimbali kuhusu hisa zao pamoja na kupata nafasi ya kutoa ushauri.
Akitoa taarifa hiyo Mwenyekiti huyo wa bodi alisema;
“Nina furaha kubwa kutangaza matokeo ya Tanzania Breweries Public Limited Company pamoja na kampuni zake tanzu kwa mwaka wa fedha ulioishia tarehe 31 Desemba 2024.
“Kampuni hii iliendelea kufanikisha mwaka mwingine wa ukuaji imara wa mapato na faida. Mapato yaliongezeka kwa asilimia 15, yakichochewa na nguvu ya bidhaa zetu kuu za bia pamoja na biashara ya vinywaji vikali.
“Usimamizi madhubuti wa mapato, ufanisi katika uzalishaji na usambazaji, pamoja na nidhamu ya matumizi ya mapato, umechangia ongezeko la faida ya uendeshaji kwa asilimia 23, sambamba na kuongezeka kwa kiwango cha faida ya uendeshaji kwa alama 1.2.
“Sekta ya vinywaji vyenye kilevi nchini Tanzania ilionesha maendeleo makubwa katika mwaka 2024. Kuimarika kwa shughuli za kiuchumi katika sekta mbalimbali pamoja na ongezeko la matumizi ya serikali kuliwezesha wananchi kuwa na kipato cha ziada, jambo lililoinufaisha sekta pamoja na kampuni.
“Mwaka 2024 tulishuhudia uwiano mzuri wa ununuzi bidhaa katika ujazo tofauti.
“Mikakati yetu iliendelea kulenga utekelezaji wa malengo yetu ya kibiashara, ambayo ni kuongoza na kukuza sekta ya vinywaji vyenye kileo nchini Tanzania, kuendelea kuboresha ufanisi wa biashara yetu na kuongeza kasi kwenye mabadiliko ya kidijitali.
“Tuliendelea kuzingatia na kuwekeza katika mauzo na masoko ya bia zetu, pamoja na ubunifu kupitia matangazo, ushirikiano wa kimkakati na kujitangaza kwenye matamasha na majukwaa mbalimbali. Mwaka 2024 tuliendelea kudhibiti zaidi ya theluthi mbili ya soko la bia nchini kupitia mkusanyiko wa chapa zetu bora na maarufu.
“Tunaendelea kuwekeza katika ubunifu ili kuongeza fursa za matumizi na kukidhi mabadiliko ya mahitaji ya walaji.
Ufanisi na ubunifu wetu katika masoko ulitambuliwa rasmi kwa timu yetu kutangazwa timu Bora ya Masoko ya mwaka na Tanzania Marketing Science Association TMSA, huku bia yetu ya Safari Lager na Konyagi zikitambuliwa kimataifa.
“Tuliendelea kusonga mbele katika mabadiliko ya kidijitali kwa kuongeza upatikanaji na matumizi ya majukwaa yetu ya kidijitali, BEES na KUJA, mfumo wa usimamizi wa usambazaji unaotumiwa na wateja wetu pamoja na vituo vya mauzo ili kuboresha ufanisi na upatikanaji wa taarifa katika kuwahudumia walaji wetu.
“Mwaka 2024 kupitia majukwaa yetu ya BEES na KUJA, tuliwaunganisha wasambazaji zaidi ya 120 moja kwa moja na wateja wa mwisho.
“Matokeo yake, bidhaa zetu sasa zinafikia kwenye takriban wauzaji wa bia rejareja 22,000 kote nchini.
“Tuliendelea kutenga rasilimali kwaajili ya kuboresha miundombinu yetu ya uzalishaji na usambazaji, tukiweka mkazo katika vifungashio vinavyorejeshwa na kuhakikisha viwanda vyetu vinaendeleza kasi ya ukuaji.
“Mwaka 2024, tulitumia jumla ya Shilingi bilioni 88.4 za Tanzania katika uwekezaji ikiwa ni pamoja na uwekezaji katika kiwanda cha Kilimanjaro Malting kilichokamilika na kuanza kufanyakazi katika robo ya mwisho ya mwaka 2024, chenye uwezo wa kuzalisha tani 8,000 za kimea cha shayiri kwa mwaka.
“Tuliendelea kutekeleza vipaumbele vyetu vya maendeleo endelevu kupitia programu za kilimo cha kisasa, vifungashio vinavyohifadhi mazingira, mipango ya kuhifadhi hali ya hewa na maji, pamoja na uwezeshaji wa ujasiriamali.
“Mwaka 2024, kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na taasisi zake mbalimbali, tuliendelea kushirikiana na wakulima wadogo katika programu zetu za kilimo cha shayiri na mtama katika maeneo ya West Kilimanjaro, Mondulina Manyara, pamoja na Dodoma.
“Kukamilika kwa kiwanda cha Kilimanjaro Malting kutatuwezesha kupanua zaidi programu za kilimo cha shayiri na kuboresha maisha ya wakulima wetu na jamii kwa ujumla.
“Katika mwaka wa 2024, asilimia 92 ya bidhaa zetu zilihifadhiwa kwenye vifungashio ambavyo vinaweza kurejeshwa au vilivyotengenezwa kwa kiasi kikubwa kutoka kwenye malighafi zinazoweza kutumika zaidi ya mara moja.
“Uwiano wa matumizi ya maji uliendelea kudhibitiwa kwa ufanisi wa lita 200 kwa kila lita 100 za bidhaa.
Tuliendelea kuhimiza unywaji wa kistaarabu kupitia kampeni mbalimbali na programu za kuelimisha jamii kuhusu unywaji wenye uwajibikaji.
“Pia, mwaka 2024, TBL Plc ilizindua mpango wa kuendeleza wauzaji wa bidhaa zetu (Retailers Development Programme) kwa lengo la kuboresha ujuzi wa biashara, uendelevu, na ufanisi wa kiutendaji kwa wafanyabiashara 22,000 wa rejareja kote nchini, ambapo wafanyabiashara 1,700 walipata mafunzo hayo ndani ya mwaka 2024.
“Ufanisi wetu wa miaka minne mfululizo hadi kufikia mwaka 2024 unatupa matumaini makubwa tunapoelekea mwaka 2025.
“Licha ya mazingira ya biashara yenye mabadiliko ya mara kwa mara, tunaendelea kuwa imara na tuna imani katika uwezo wa timu yetu kutekeleza mikakati yetu ya kibiashara na kufikia malengo ya ukuaji endelevu. Sekta ya vinywaji vya kilevi nchini “Tanzania inaendelea kukua na kubaki kuwa muhimu. Tunaahidi kuendelea kuongoza katika sekta hii kupitia bidhaa bora na zinazoongoza sokoni.
“Tutaendelea kuwaweka wateja na walaji wetu katikati ya kila jambo tunalofanya. Tumejizatiti kufanikisha ukuaji endelevu na wenye tija kupitia uwekezaji unaoendelea katika chapa zetu, miundombinu ya uzalishaji, uwezo wa usambazaji na mabadiliko ya kidijitali.
“Kwa kumalizia, napenda kutoa shukrani za dhati kutoka kwa Bodi ya Wakurugenzi kwa wateja wetu wote waaminifu na washirika wetu wa kibiashara. Tunawashukuru kwa dhati wafanyakazi na menejiment kwa bidii yao na utekelezaji wa mikakati ya kibiashara kwa mwaka mwingine kwa mafanikio.
“Vilevile, napenda kuwashukuru wanahisa wetu wote kwa msaada wao wa kudumu, na Bodi kwa kuendeleza viwango vya juu vya uongozi na utawala bora wa kampuni.
“Mwisho, tunaitambua na kuithamini sana Serikali yetu kwa mchango wake mkubwa katika kuweka mazingira bora ya kufanyabiashara. Tunaahidi kuendelea kushirikiana nayo kwa maendeleo ya pamoja. Alimaliza kusema Leonard Mususa Mwenyekiti huyo wa Bodi ya Wakurugenzi Tanzania Breweries Public Limited Company (TBL Plc)