Dar es Salaam, Tanzania – Mwanaharakati maarufu wa kimataifa wa haki ya elimu, Mshindi wa Tuzo ya Amani ya Nobel na Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa, Malala Yousafzai (pichani), anatarajiwa kuwasili nchini Tanzania wiki hii kwa ziara ya kikazi ya siku kadhaa kwa mwaliko wa Global Partnership for Education (GPE), ambayo Mwenyekiti wake ni Rais Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete.
Hii itakuwa ni mara ya kwanza kwa Malala kutembelea Tanzania, ambapo atashiriki shughuli mbalimbali zinazolenga kuhamasisha haki ya elimu kwa watoto, hususan wasichana. Akiwa nchini, Malala atakutana na viongozi wa serikali, wadau wa sekta ya elimu, na kujionea namna elimu, sanaa na michezo vinavyotumika kama njia ya kukuza mwamko wa elimu katika jamii.
Akizungumza kuhusu ziara hiyo, Malala amesema:
“Hii ni mara yangu ya kwanza kufika nchini Tanzania. Nitasherehekea Siku ya Malala pamoja na jamii kwa kuonesha mshikamano na wasichana wa Tanzania, kupaza sauti zao na kujifunza kutoka kwenye mafanikio yao.”
Tarehe 12 Julai ambayo ni siku ya kuzaliwa kwa Malala, imekuwa ikiadhimishwa kimataifa kama Siku ya Malala Duniani tangu mwaka 2013, kufuatia hatua ya Umoja wa Mataifa kuenzi mchango wake mkubwa katika kupigania haki ya elimu kwa wasichana – harakati ambazo zilimfanya kushambuliwa kwa risasi na kundi la Taliban akiwa njiani kurejea nyumbani kutoka shule akiwa na umri wa miaka 15.
Katika ziara hii, Malala atakuwa pia anatekeleza majukumu yake kupitia Malala Fund, taasisi aliyoiunda pamoja na Shiza Shahid yenye lengo la kupigania upatikanaji wa elimu bora kwa wasichana kote duniani.
Kuhusu Malala Yousafzai
Malala alizaliwa tarehe 12 Julai 1997 huko Swat, Pakistan. Alianza harakati za kutetea elimu akiwa na umri wa miaka 11 kwa kuandika blogu kupitia BBC Urdu chini ya jina la “Gul Makai,” akielezea maisha ya wasichana chini ya utawala wa Taliban. Mwaka 2012, alijeruhiwa kwa kupigwa risasi kichwani na Taliban kutokana na harakati zake, tukio lililoibua mshikamano mkubwa wa kimataifa.
Alihamia Uingereza kwa matibabu, akaendelea na masomo na harakati zake za kimataifa, na kisha kuhitimu Shahada ya Falsafa, Siasa na Uchumi (PPE) katika Chuo Kikuu cha Oxford mwaka 2020. Ametunukiwa tuzo mbalimbali ikiwemo Sakharov Prize, uraia wa heshima wa Canada, na kutajwa mara kadhaa na jarida la TIME miongoni mwa watu 100 wenye ushawishi mkubwa duniani.
Kuhusu Global Partnership for Education (GPE)
GPE ni mfuko mkubwa zaidi wa kimataifa unaojikita kikamilifu katika kuimarisha sekta ya elimu katika nchi zenye kipato cha chini. Kwa zaidi ya miongo miwili, GPE imekuwa ikitoa rasilimali na usaidizi wa kimkakati kujenga mifumo imara ya elimu, kwa lengo la kuhakikisha watoto wengi zaidi – hususan wasichana – wanapata elimu wanayohitaji ili kustawi na kuchangia katika maendeleo ya dunia.
GPE huleta pamoja serikali, wafadhili, mashirika ya kimataifa, asasi za kiraia, vyama vya walimu, vijana na sekta binafsi katika juhudi za pamoja za kuleta mageuzi ya elimu.