Na John Bukuku, Dar es Salaam
Serikali imepongezwa kwa kuendelea kuweka mazingira wezeshi kwa wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, hatua ambayo imeiwezesha Mamlaka ya Masoko ya Mitaji na Dhamana (CMSA) kutoa idhini kwa kampuni ya I Trust Finance kuanzisha mfumo mpya wa uwekezaji wa fedha za kigeni uitwao I Dollar.
Pongezi hizo zimetolewa leo, Julai 10, 2025, jijini Dar es Salaam na Afisa Mtendaji Mkuu wa CMSA, Mhe. Nicodemus Mkama, katika hafla ya uzinduzi wa mfuko huo, ambao unalenga kuwapa Watanzania fursa ya kuwekeza fedha za kigeni kwa kiwango cha chini kuanzia dola moja (USD 1), huku faida ikitolewa pia kwa fedha ya kigeni.
“Tunaipongeza serikali kwa kuendelea kuweka mazingira rafiki ya uwekezaji, jambo ambalo limeiwezesha CMSA kutoa idhini kwa I Trust Finance kuanzisha mfuko huu wa kwanza wa aina yake unaowezesha Watanzania kuwekeza moja kwa moja katika fedha za kigeni,” alisema Mkama.
Aidha, Mhe. Mkama ametoa rai kwa wawekezaji wa Kitanzania—wakiwemo watu binafsi, taasisi, na kampuni—kuchangamkia fursa hii kwa ajili ya kukuza mitaji yao na kupata faida kwa njia salama na ya kimataifa.
Kwa upande wake, mmoja wa Wakurugenzi wa I Trust Finance, Prof. Mohamed Warsame, amewataka Watanzania kuzingatia sheria mpya ya nchi inayokataza matumizi ya dola za Kimarekani katika shughuli za malipo ya huduma ndani ya nchi, badala yake kuzitumia fedha hizo katika uwekezaji kupitia I Dollar.
“Kama mnavyofahamu, sheria ya nchi imebadilika mwaka huu. Watanzania, taasisi, mashirika na watu binafsi hawaruhusiwi tena kutumia dola za Kimarekani moja kwa moja katika malipo ya huduma. Hivyo basi, ni vyema fedha hizo zikaelekezwa katika mifuko ya uwekezaji kama I Dollar, ambayo inaleta manufaa zaidi kwa wananchi na taifa,” alisema Prof. Warsame.