:::::::::
Mwenyekiti wa Bodi ya Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA), Dkt. Leonard Akwilapo, amesema kuwa Mamlaka ya Elimu Tanzania (TEA) imejipanga kikamilifu kutekeleza miradi ya ujenzi wa miundombinu kwa ajili ya mafunzo ya amali ili kuweka mazingira wezeshi ya utoaji wa mafunzo hayo nchini.
“Sisi kama Mamlaka ya Elimu Tanzania tumepewa fedha za kutosha kwa ajili ya kutekeleza miradi ya miundombinu ya mafunzo ya amali katika shule zilizoteuliwa kutoa mafunzo hayo,” alisema Dkt. Akwilapo.
Dkt. Akwilapo alitoa kauli hiyo alipokuwa akizungumza mara baada ya kutembelea banda la TEA katika Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Saba Saba, yanayofanyika jijini Dar es Salaam.
Aidha, alitumia fursa hiyo kumshukuru Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, kwa kuendelea kuipatia TEA fedha kupitia Mfuko wa Elimu wa Taifa, ambazo zimewezesha utekelezaji wa miradi mbalimbali ya elimu.
Alibainisha kuwa TEA itaendelea kufadhili miradi ya uboreshaji wa miundombinu ya mafunzo ya amali katika shule za sekondari na vyuo nchini, ili kuimarisha ubora wa elimu ya vitendo.
Vilevile, Dkt. Akwilapo alizungumzia utekelezaji wa Mradi wa Mfuko wa Kuendeleza Ujuzi (SDF) unaoratibiwa na kusimamiwa na TEA, ambao umewawezesha maelfu ya vijana kupata mafunzo yanayowawezesha kujiajiri na kujipatia kipato.
Akiwa katika banda la TEA, alipata fursa ya kuzungumza na baadhi ya wanufaika wa mafunzo hayo waliofadhiliwa kupitia SDF, ambao walieleza namna mafunzo hayo yalivyobadilisha maisha yao.
TEA imeshiriki Maonyesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa kwa lengo la kutoa elimu kwa umma kuhusu majukumu yake, pamoja na kujenga mahusiano na wadau muhimu ili kuimarisha ushirikiano wa kikazi.