Wananchi 3,529 ikiwa ni wanaume 1,630 na wanawake 1899 wamepata elimu na huduma za msaada wa kisheria ndani ya banda la Wizara ya Katiba na Sheria pamoja na migogoro zaidi ya 500 kupokelewa na kushughulikiwa katika maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2025).
Waziri wa Katiba na Sheria Dkt Damasi Ndumbaro amebainisha hayo leo Julai 11,2025 mara baada ya kutembelea mabanda yanayohusika na mfumo wa haki jinai na haki madai pamoja na banda la Wizara ya Katiba na Sheria.
Waziri Dkt Ndumbaro ameeleza kuwa katika banda la Wizara hiyo wananchi wanapata elimu ya sheria, elimu ya katiba pamoja na msaada wa kisheria ambapo pia naye ameweza kuwahudumia wananchi kwa kusikiliza migogoro yao na kuitatua hapo kwa hapo.
“Napenda kuwajulisha wananchi wa Dar es Salaam kuwa huduma ya msaada wa kisheria itaendelea kutolewa bure hadi tarehe 13, Julai 2025 katika banda letu la Wizara, wataalamu wa sheria wametumwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. Samia Suluhu Hassan aje kuwahudumia wananchi wote bure”, amesisitiza Waziri Dkt. Ndumbaro.
Aidha ametoa pongezi kwa Katibu Mkuu Wizara ya Katiba na Sheria Eliakim Maswi pamoja na viongozi wote wa Wizara kwa jitihada zao ambazo zimewezesha wizara hiyo kushika nafasi ya kwanza kati ya Wizara zote zilizoshiriki maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Dar es Salaam (Sabasaba 2025).
Waziri Dkt Ndumbaro ameongeza kuwa Wizara kwa sasa inaenda kumfuata mwananchi na kumsogezea huduma za msaada wa kisheria ambapo huduma hiyo imekosekana kwa miaka mingi huku akieleza kuwa migogoro mingi iliyopokelewa ni ya ardhi, mirathi, ndoa, ukatili wa kijinsia, kesi za jinai pamoja na madai.