Na: Happiness Sam – Dar es Salaam
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini TANAPA – Jenerali mstaafu George Waitara amewahamasisha wawekezaji kuwekeza katika mazao ya utalii pamoja na malazi hususani katika Hifadhi za Kusini zilizojaliwa kuwa na hazina lukuki ya wanyamapori ili kuvutia watalii wengi kwa lengo la kuliongezea Taifa mapato.
Hayo aliyasema leo Julai 12, 2025, alipotembelea Banda la Wizara ya Maliasili na Utalii katika Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa ya Sabasaba yanayoendelea jijini Dar es Salaam.
Jenerali Waitara alisema, “Ukanda wa Kusini una hazina kubwa ya vivutio vya kipekee ambavyo vinaweza kuwa kichocheo kikubwa cha uchumi na utalii endapo vitawekewa nguvu ya uwekezaji na kutangazwa kikamilifu, ni muda muafaka sasa kwa sekta binafsi kushirikiana na Serikali kupitia TANAPA katika kuibua na kuendeleza maeneo hayo, ili kupanua wigo wa kitalii na kuongeza pato la Taifa kupitia sekta hiyo”.
“Kama ilivyozoeleka wawekezaji wengi wa sekta ya utalii wamewekeza sana upande wa Kaskazini katika mikoa ya Arusha na Kilimanjaro. Ni wakati sasa wa kugeukia Hifadhi za Kusini katika mikoa ya Iringa, Mbeya, Njombe na Katavi ili watalii wetu wagawanyike kwa ajili ya kupata vionjo na ladha tofauti ya utalii wa kitamaduni kwa makabila ya wahehe, Wangoni, Wagongwe na makabila mengine ya Kusini, pia waonje mazingira mengine yenye vivutio tofauti na vilivyopo katika maeneo ya Kaskazini. Kwa kufanya hivyo tutapunguza msongamano wa watalii eneo moja na mapato ya utalii kuelekea maeneo ya Kusini pia.”
Vilevile Jenerali Waitara aliongeza kuwa Hifadhi za kusini kama Ruaha ilishinda tuzo ya kivutio bora cha kiutamaduni barani Afrika, na Kitulo ikinyakua tuzo ya eneo bora la fungate Afrika, hivyo sifa hizi na nyingine kedekede zinatarajia kuleta watalii wengi ndio maana tunawasisitiza kuwekeza upande huo kwani wawekezaji hawatajutia fedha zao walizowekeza.
Aidha, Waitara alieleza kuwa zaidi ya watu elfu sita wamepita kutembelea banda la Wizara ya maliasili na utalii katika maonesho hayo, hatua inayodhihirisha mwitikio chanya wa wananchi katika kujifunza masuala ya uhifadhi na utalii.
Naye, Kamishna Msaidizi wa Uhifadhi TANAPA, Neema Mollel, alisema kuwa TANAPA imetumia fursa ya maonesho hayo kama jukwaa la kutoa elimu kwa umma, kutangaza vivutio vya utalii pamoja na kutangaza fursa za uwekezaji zinazopatika katika Hifadhi za Taifa.
Maonesho ya 49 ya Biashara ya Kimataifa Sabasaba yalianza rasmi Juni 28, na yanatarajiwa kufungwa kesho Julai 13, huku yakibeba kaulimbiu inayosema “Maonesho ya Kibiashara ya Kimataifa Sabasaba, Fahari ya Tanzania.”