Kibaha, Pwani – July 08, 2025
Serikali imetangaza rasmi kupandisha hadhi ya Halmashauri ya Mji wa Kibaha kuwa Manispaa ya Kibaha kuanzia tarehe 20 Juni 2025. Uamuzi huu ni sehemu ya mkakati wa serikali kuboresha utoaji wa huduma kwa wananchi na kuharakisha maendeleo ya miji inayokua kwa kasi nchini.
Tangazo hilo limepokelewa kwa shangwe na matumaini makubwa na wakazi wa Kibaha, ambao sasa wanatazamia kunufaika na fursa mbalimbali zitakazotokana na hadhi hiyo mpya.
Akizungumza na wadau wa maendeleo, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kibaha Dkt Rogers Shemwelekwa amewata Wananchi na wadau wa maendeleo manspaa ya kibaha Kwa Tayari na kuendana na Kasi ya maendeleo ya Manspaa ili kujiletea maendeleo.
“Kupandishwa hadhi kwa Kibaha kuwa Manispaa ni ushahidi wa kazi kubwa iliyofanywa na wananchi na viongozi wao kwa pamoja. Tunakwenda kushuhudia maboresho ya miundombinu, huduma bora kwa wananchi, pamoja na ongezeko la ajira na fursa za kiuchumi.”
Amezitaja faida ya Halmashauri ya mji kupandishwa hadhi kuwa Manspaa ni
1. Miundombinu Bora:
Manispaa itapata bajeti kubwa zaidi kwa ajili ya ujenzi na ukarabati wa barabara, masoko, stendi za mabasi, mifereji ya maji, na taa za barabarani. Hii itarahisisha usafiri na biashara katika maeneo yote ya Kibaha.
2. Huduma Bora za Jamii:
Huduma za afya, elimu, na usafi wa mazingira zitaboreshwa. Shule na vituo vya afya vitapewa vifaa, watumishi na miundombinu ya kisasa ili kuhudumia wananchi kwa ufanisi zaidi.
3. Fursa za Ajira:
Miradi ya maendeleo na uwekezaji itakayotekelezwa italeta ajira kwa vijana na wanawake wa Kibaha, ikiwemo sekta ya ujenzi, biashara, na huduma.
4. Uwekezaji na Biashara:
Hadhi ya manispaa huvutia wawekezaji wa ndani na nje. Hii inamaanisha kujengwa kwa viwanda, maduka makubwa (supermarkets), hoteli, na huduma nyingine za kisasa zitakazoinua uchumi wa eneo hili.
5. Ushiriki wa Wananchi na Uwajibikaji:
Kwa kuwa Manispaa inakuwa na mifumo madhubuti ya usimamizi, wananchi watashirikishwa zaidi katika mipango ya maendeleo kupitia vikao vya kisheria na kamati za mtaa. Uwajibikaji wa viongozi utaimarika.
6. Kuongezeka kwa Mapato ya Ndani:
Kwa kuwa na vyanzo vingi vya mapato kama ushuru, tozo na ada halali, Manispaa itakuwa na uwezo mkubwa wa kugharamia miradi ya kijamii bila kutegemea sana misaada ya nje.
Mmoja wa wakazi wa Kibaha, Mzee Mfinanga (Njuweni), amesema:
“Kupandishwa hadhi ni kama tumepata mwanga mpya. Tunategemea kuona mabadiliko ya kweli, hasa barabara nzuri, huduma bora za afya na elimu kwa watoto wetu.”
Serikali imesisitiza kuwa hatua hii inakwenda sambamba na ajenda ya maendeleo kwa vitendo, na imetoa wito kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda na kuendeleza mafanikio haya.