Na John Mapepele
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan ametunukiwa tuzo maalum ya kutambua mchango wake kwenye Sekta ya Afya na Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri hii leo.
Tuzo hiyo ameitoa Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI, Mhe. Mohamed Mchengerwa kwa niaba ya Waganga hao na kumkabidhi Makamo wa Rais, Mhe. Dkt. Philipo Mpango aliyekuwa mgeni rasmi katika Mkutano huo wa Mwaka wa Waganga Wakuu wa Mikoa na Halmashauri jijini Dodoma.
Mbali na tuzo hiyo pia Waganga Wakuu wamemtunukia Makamo wa Rais tuzo hiyo pamoja na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais-TAMISEMI Mhe Mohamed Mchengerwa na Waziri wa Afya Mhe. Jenista Mhagama.
Mhe. Mpango amewapongeza Waganga Wakuu nchini kwa kazi wanayofanya ya kuwahudumia wananchi huku akiwataka waendelee kuimarisha huduma na sekta ya afya kwa ujumla na kuzingatia maadili ya taaluma yao.

Amesisitiza kuwa Serikali itatekeleza mara moja maombi ya kuboresha stahili za wataalam hao kulingana hali halisi ya uchumi.
“Nawaelekeza Mawaziri wa Afya na OR-TAMISEMI kwa kushirikiana na Waziri wa Fedha washughulikie suala la ucheleweshaji wa posho za madaktari na wahudumu wa afya.” Amesisitiza Mhe. Mpango
Amesema kwa sasa Serikali inapoelekea kutekeleza mpango wa Bima ya Afya kwa Wote Mamlaka za Serikali za Mitaa zinatakiwa kuhakikisha zinasimamia vema ukusanyaji wa mapato na kuhakikisha yanatumika kiadilifu ili kuboresha zaidi utoaji wa huduma.
Pia amewapongeza Wakuu wa Mikoa na Wilaya, pamoja na Wakurugenzi wa Halmashauri/Manispaa na Majiji kwa kusimamia utekelezaji wa miradi ya maendeleo, ikiwemo ile ya afya na vifaa tiba katika Halmashauri/Manispaa/Majiji.
Amesema ili kuimarisha huduma za afya na usimamizi shirikishi, Serikali imenunua na kusambaza magari ya kubeba wagonjwa (ambulance) na mashine za kisasa za kidijiti (Digital X-ray na ultrasound) na kuagiza kuvitunza vifaa hivyo na vingine vitakavyonunuliwa ili viweze kutumika kwa muda mrefu na kutoa huduma kwa watu wengi zaidi.
Akimkaribisha Mhe. Mpango kutoa hotuba, Mhe.Mchengerwa amemshukuru Rais Samia kwa maono yake makubwa na miongozo kwenye sekta ya afya ambayo yameleta mapinduzi makubwa katika kipindi kifupi.
Mhe. Mchengerwa ametumia mkutano huo kutaja mafanikio lukuki yaliyopatikana katika kipindi hiki.
Aidha, amesema mafanikio hayo pia yanatokana na ushirikiano baina ya Wizara yake na Wizara ya Afya.
Katika mkutano huo wadau mbalimbali ya afya pia wametunukiwa vyeti vya kutambua michango yao.